Profesa Assad asisitiza hakuondolewa kihalali, akerwa kuitwa mstaafu

Profesa Assad asisitiza hakuondolewa kihalali, akerwa kuitwa mstaafu

Muktasari:

  • Profesa Assad amesema ziko njia za kumuondoa CAG ambazo kwake hazikufuatwa hivyo neno mstaafu linamuudhi linaposikika masikioni mwake.

Dodoma. Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa zamani, Profesa Mussa Assad amesema hapendi kuitwa Mstaafu na neno hilo linamchukiza, akidai kuwa taratibu za kumwondoa hazikufuatwa.

Profesa Assad ameyasema hayo leo Oktoba 6 jijini Dodoma wakati wa mdahalo juu ya kitabu cha Rai ya Jenerali kinachozungumzia umuhimu wa Katiba Mpya.

Hata hivyo taarifa iliyotolewa na Serikali mwaka 2019 ilieleza kuwa Profesa Assad kipindi chake kilimalizika Novemba 4, 2019

"Sipendi sana kusikia neno mstaafu na kwamba neno hilo linaniudhi linapotamkwa mbele yangu," amesema Profesa Assad.

Profesa Assad aliteuliwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwa CAG Novemba 5, 2014 na aliondolewa Novemba 4, 2019 kwa maelezo kuwa alimaliza muda wake.

Kabla ya kuondolewa kwake, ulizuka mvutano kati yake na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, uliosababisha Profesa Assad kufikishwa kwenye Kamati ya Bunge ya Haki, aadili na madaraka ya Bunge akidaiwa kudharau mhimili huo kwa kauli yake kuwa Bunge ni dhaifu.

Mdahalo huo umeandaliwa na kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC) na wasemaji ni Jenerali Ulimwengu na Profesa Mussa Assad huku makundi mbalimbali ikiwemo wabunge wameshiriki.

Amesema kuondolewa kwake hakukuwa na Sababu isipokuwa kulitokana na kutosimamiwa vema kwa Katiba ya nchi licha ya kutaja namna nzuri ya kumuondoa mtu wa cheo hicho.

Assad ambaye leo ametimiza miaka 60, amesema kwa sasa maisha yake ni mazuri baada ya kuamua kusimamia kile anachokiamini kuliko kuwa na unafiki kama baadhi ya watu wanaotaka kujipendekeza kwa sababu ya kuwa na magari V8.