Profesa Kabudi: Lindeni vyanzo asili vya maji, epukeni makazi holela
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza jijini Dodoma leo Julai 2, 2026. Picha na Elidaima Mangela
Muktasari:
- Profesa Kabudi amesema ongezeko makazi holela katika baadhi ya maeneo ni miongoni mwa sababu zinazochangia uharibifu wa vyanzo vya maji, ikiwemo mito, chemchemi, mabwawa ya asili na kuwa chanzo cha magonjwa.
Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi ametoa wito kwa wananchi kulinda vyanzo vya asili vya maji ili visichafuliwe wala kuharibiwa na shughuli za kibinadamu.
Prefesa kabudi ametoa wito huo leo Alhamisi, Julai 2, 2026 jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa kongamano la pili la wadau wa usafi wa mazingira lililoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Profesa Kabudi amesema ongezeko la makazi holela katika baadhi ya maeneo ni miongoni mwa sababu zinazochangia uharibifu wa vyanzo vya maji, ikiwemo mito, chemchemi na mabwawa ya asili.
“Ujenzi wa makazi na yasiofuata mpangilio unapelekea unaharibu vyanzo vya maji na kupunguza ubora wa maji jambo litakaoathiri afya za wananchi na shughuli za kiuchumi zinazotegemea vyanzo vya maji,” amesema Profesa Kabudi.
Waziri amesema endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kukabiliana na changamoto hiyo, jamii inaweza kukumbwa na ongezeko la magonjwa yatokanayo na uchafuzi wa mazingira na kuathiriwa kwa mchakato wa uzalishaji wa mazao yatokanayo na vyanzo vya maji kama mabwawa ikiwemo nishati ya umeme.
“Mabwawa yaliojengwa, yanategemea vyanzo asili vya maji vilivyopo kwenye maeneo yetu hivyo visipolindwa havitazalisha kile tulichokitarajia wakati wa ujenzi wake,” amesema Profesa Kabudi.
Amesisitiza kuwa upo umuhimu wa kila mwananchi kushiriki katika kulinda mazingira ili kuhakikisha rasilimali maji zinadumu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Profesa Kabudi ametoa wito kwa mamlaka za serikali za mitaa kuimarisha mipango miji na kusimamia ipasavyo matumizi ya ardhi ili kudhibiti makazi holela akisisitiza kuwa ulinzi wa mazingira ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu na ustawi wa Taifa kwa ujumla.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya maji na mazingira, Kunti Majala ametoa wito kwa wazazi na watu wazima kuwalinda watoto dhidi ya athari uchafuzi wa mazingira kwa kuimarisha usafi kwenye maeneo na kuacha kutupa uchafu, ili kuondoa athari za kiafya zinazoweza kuwakumba watoto hao.
Kunti amesema uchafuzi wa mazingira unaofanywa na watu wazima na wazazi ikiwemo kutupa taka huwaathiri zaidi watoto waliopo kwenye mazingira kutokana na kukosa uelewa juu ya namna ya kujikinga na athari hizo.
Hivyo, amesema ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha watoto wanaishi kwenye mazingira safi na salama kwa kuwafundisha kanuni za usafi wa mazingira na kuepuka kutupa taka katika mazingira hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Shekimweri amezitaka taasisi zisizo na miundombinu ya kutibu taka kinyesi na kujenga miundombinu hiyo ili kuongeza ufanisi katika uvunaji wa nishati inayotokana na rasilimali hiyo.
Shekimweri amesema hatua hiyo pia itasaidia kukabiliana na athari za kimazingira zinazoweza kusababishwa na udhibiti usio sahihi wa taka hizo ikiwemo magonjwa ya mlipuko na uchafuzi wa mazingira.