Profesa Mkumbo: Wanawake tumieni fursa mikoani

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Serikali imewataka wanawake kuchangamkia fursa zinazotolewa katika mikoa wanayoishi ili kutatua changamoto zinazowakabili.

Dar es Salaam. Serikali imewataka wanawake kuchangamkia fursa zinazotolewa katika mikoa wanayoishi ili kutatua changamoto zinazowakabili.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Machi 5, 2021 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo wakati anazindua maonyesho ya biashara na wanawake Tanzania yanayofanyika Mlimani City.

Mkumbo ambaye ni mbunge wa Ubungo amesema Serikali kwa kutambua umuhimu na mchango wa maendeleo ya wanawake kwa Taifa,  wameanzisha dirisha maalumu la mikopo kwa halmashauri zote nchini kwa ajili ya kuwainua wanawake na vijana.

"Tunatambua jitihada zenu na malengo yenu lakini Serikali tunatoa wito kwa wanawake wote nchini kuchangamkia fursa zinazotolewa kupitia mikoa yenu ziweze kuwakwamua kwenye changamoto zinazowakabili,” amesema Mkumbo.

Waziri huyo amebainisha kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kupitia mifuko mbalimbali kisheria na kuiboresha lengo likiwa ni kuwainua wafanyabiashara wadogo ikiwemo wanawake na vijana.

Mkurugenzi wa Chama cha Wafanyabiashara  Tanzania (Tabwa), Noreen Mawalla aliiomba Serikali kuwasaidia majengo ya wazi ili wanawake wafanyie biashara zao katika mazingira mazuri na salama yatakayowawezesha kulipa kodi kwa wakati.


Imeandikwa na Tuzo Mapunda