Profesa Ngowi azikwa Moshi
Muktasari:
- Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi aliyefariki dunia Machi 28, 2022 amezikwa leo kijijini kwao Singa kati, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Moshi. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi aliyefariki dunia Machi 28, 2022 amezikwa leo kijijini kwao Singa kati, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Mapadre 50 wa jimbo Katoliki la Moshi wameshiriki ibada ya mazishi iliyofanyika katika kanisa la Singa-Kibosho, wilayani humo.
Akitoa salama za rambirambi wakati wa ibada ya mazishi, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima amesema kanisa katoliki halitasahau kamwe mchango wake.
"Katika kamati mbalimbali Profesa Ngowi alikuwa na mchango mkubwa na alikuwa na unyenyekevu mkubwa kwa viongozi wa dini wakati akitoa mafunzo nyakati mbalimbali" amesema Dk Kitima
Akizungumza kwa niaba ya Askofu wa Jimbo hilo, Padre Deogradius Matiika amesema Profesa Ngowi alikuwa ni msaada mkubwa kwenye shughuli mbalimbali za kanisa na maendeleo.
"Temepoteza mtu muhimu sana katika maendeleo. Katika historia yake na mambo makubwa ambayo ameyafanya katika nchi hii, hakika hajafa na ataendelea kuishi tuendelee kumwombea ili yale mazuri aliyoyafanya yaendelee kuenziwa,"amesema Padre Matiika
Profesa Ngowi ameacha watoto watatu na mke mmoja.