Raia 47 wa Ethiopia wakamatwa tena Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu akiwa na kamati ya usalama ya mkoa huo katika makao makuu wa ofisi za Jeshi la Polisi mkoani humo ambapo wahamiaji hao haramu  47 raia wa Ethiopia wanakoshikiliwa. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

Wahamiaji hao haramu 47 raia wa Ethiopia wamekamatwa leo Agosti 11 wakipita njia za panya katika eneo la Mgagao, Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro, wakisema wanaelekea nchi ya Afrika Kusini kutafuta maisha.

Moshi. Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la uhamiaji mkoani Kilimanjaro wamefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 47 raia wa Ethiopia walioingia nchini kwa njia za panya katika eneo la Mgagao wilayani Mwanga.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 11, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Edward Mwenda amesema wahamiaji hao wamekamatwa usiku wa kuamkia leo katika operesheni maalumu inayoendelea mkoani humo.

"Katika operesheni maalum ambayo imefanyika katika mkoa wetu usiku wa kuamkia leo tumewakamata raia wa Ethiopia 47, akiwemo msafarishaji mmoja wa Tanzania ambaye tunamshikilia kwa mahojiano zaidi.

"Mkoa huu wa Kilimanjaro una njia nyingi za panya na hivyo raia hawa wameingia nchini bila vibali kwa kupitia njia za panya, hivyo tumefanikiwa kuwakamata leo kutokana na kazi kubwa ambayo tumeifanya kwa weledi na uzalendo wa hali ya juu," amesema Mwenda.

Kamishna Mwenda amesema baada ya kuwakamata na kuwahoji wahamiaji hao wamedai walikuwa wanapita kwa njia za panya kupitia nchini Tanzania kuelekea nchi ya Afrika kusini kwenda kutafuta maisha.

Naye Kamanda wa Polisi mkoani humo, Simon Maigwa amesema wanaendelea kuwashikilia na kuwahoji wahamiaji hao pamoja na Mtanzania mmoja na kusema kwamba jeshi hilo limejipanga kuhakikisha linafanya kazi usiku na mchana ili kukamata mtandao wa usafirishaji haramu wa binadamu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amevipongeza vyombo hivyo vya ulinzi na usalama mkoani humo kwa kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha wale wanaovunja sheria za nchi wanakamtwa na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

"Huyu Mtanzania tutamshughulikia ili aone sheria za nchi na taratibu zake zipo kwasbabu sasa hivi ungekuta anafanya kazi inayozalisha na sio kusafirisha wahamiaji hawa, navipongeza vyombo vyangu vya usalama kwa kufaya kazi nzuri na kwa weledi," amesema RC Babu.

Aidha amewapongeza wananchi wa mkoa huo hasa wale wanaoishi mipkani kwa kuendelea kuwa wazalendo na kutoa ushirikiano mkubwa kwenye vyombo vya usalama.