Rais Biden ‘ampindulia meza’ Trump

Rais Joe Biden wa Marekani akihutubia Bunge

Muktasari:

  • Katika hotuba yake ya mwaka, Rais Joe Biden amekiri kuwa ni mzee lakini amesisitiza kwamba anajua kinachostahimili na kwamba suala muhimu ni umri wa mawazo.

Washington. Rais Joe Biden wa Marekani amejibu kauli za mpinzani wake, Donald Trump, kuhusu umri wake na ufanisi wake.

Biden amesisitiza kwamba suala sio umri wake, bali ni mawazo na uongozi wake wa kisiasa.

Katika hotuba yake ya mwaka, amekiri kuwa ni mzee lakini amesisitiza kwamba anajua kinachostahimili na kwamba suala muhimu ni umri wa mawazo.

Trump, ambaye anawania kurejea madarakani, amekuwa akimshambulia Biden kwa kudai kuwa amepungua nguvu na kumbukumbu. Biden amejibu mapigo kwa kusema kuwa, licha ya umri wake, yeye bado ni kiongozi imara na mwenye uwezo wa kuongoza Marekani.

Kwenye hotuba yake, Biden amekumbusha mafanikio ya Serikali yake katika miundombinu na uzalishaji wa bidhaa.

Aidha, ametoa mapendekezo ya kuongeza ushuru kwenye mafuta ya usafiri wa ndege za kibinafsi, hatua inayoweza kuathiri wapinzani wake, akiwemo Trump.

Pamoja na hayo, hotuba ya Biden ilikumbwa na upinzani ndani na nje ya ukumbi wa Bunge.

Wafuasi wa Palestina walipinga sera za Biden kuhusu Israel, huku baba mzazi wa mwanajeshi aliyekufa nchini Afghanistan, akikamatwa baada ya kufanya vurugu na kumlaumu Biden kwa kifo cha mwanawe.

Hali hii inajiri wakati uchaguzi mkuu ukiwa unakaribia, ambapo Biden anatafuta muhula wa pili na anaweza kukutana tena na Trump, ambaye anajaribu kurudi tena kwenye ulingo wa kisiasa.

Uchaguzi huo unaweza kuleta mabadiliko katika mwelekeo wa siasa za Marekani.

Imeandikwa na Noor Shija