Rais Dk Mwinyi ataka nchi za Afrika kuimarisha ulinzi, haki za binadamu
Muktasari:
- Oktoba 21 kila mwaka, Bara la Afrika linaadhimisha Siku ya Haki za Binadamu Afrika na kaulimbiu ya mwaka huu wa 2023 ni “Kuimarisha na Kuendeleza Utamaduni wa Haki za Binadamu kwa Nyakati zijazo.
Arusha. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amezitaka nchi za Bara la Afrika na taasisi za haki za binadamu kuendelea kuchukua hatua za kuimarisha ulinzi na utetezi wa haki za binadamu.
Aidha amezitaka nchi hizo kuchukua hatua stahiki katika kukabiliana na changamoto za ulinzi na uhifadhi wa haki za binadamu ambazo bado zinakabili nchi hizo ikiwemo mapinduzi ya serikali zilizo madarakani na vita vya wenyewe kwa wenyewe na kushirikiana katika kuyakabili matukio mbalimbali yanayohitaji msaada wa kibinadamu barani humo.
Rais Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 20, 2023 jijini Arusha, kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan akifungua kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.
Amesema suala la ulinzi na uhifadhi wa haki za binadamu katika bara la Afrika kwa jumla, bado kwa kiasi fulani linakabiliwa na changamoto, ikiwemo mapinduzi ya Serikali zilizo madarakani, vita vya wenyewe kwa wenyewe, mila na desturi zisizofaa, ukatili wa kijinsia, athari hasi za utandawazi na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu haki zao.
"Nitoe wito kwa Serikali mbalimbali na Taasisi za haki za binadamu kuendelea kuchukua hatua za kuimarisha ulinzi na utetezi wa haki za binadamu na kushughulikia kikamilifu changamoto zilizopo na kuchukua hatua stahiki katika kukabiliana na changamoto hizo," amesema.
"Kwa ujumla, Bara la Afrika na Tanzania kwa umahususi wake tunaheshimu haki za binadamu kwa kuzingatia utamaduni, maadili na tunu zetu kama Waafrika,” amesema.
Kuhusu Tanzania amesema inatekeleza na kusimamia haki za binadamu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria, kanuni na taratibu zilizopo na kuwa katika kuhakikisha wanazilinda haki za binadamu na watu wameanzisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora yenye lengo la kutetea, kulinda na kuhifadhi haki za binadamu.
"Katika katiba yetu, haki za binadamu zimeainishwa kuanzia Ibara ya 12 hadi 24 lakini pia Katiba yetu kuanzia Ibara ya 25 hadi 30 imeainisha wajibu wa kila raia na jitihada mbalimbali zimechukuliwa na Serikali ili kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kutekelezwa kwa mujibu wa mikataba ambayo Tanzania ni mwanachama," amesema.
Dk Mwinyi amesema jitihada za Tanzania zimeboresha hali ya upatikanaji wa haki mbalimbali ikiwemo haki ya usawa mbele ya sheria, afya, elimu, maji na mazingira safi, uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kuabudu, ajira, haki ya kumiliki mali na uhuru wa vyombo vya habari.
"Kwa taarifa ni kwamba, kutokana na uhuru huo, hivi sasa Tanzania ina vyombo vya habari vingi vikiwemo redio 210, televisheni 56, magazeti 288 pamoja na mitandao mbalimbali ya kijamii, pia tumefikia hatua kubwa ya kuimarika kwa uhuru wa kidemokrasia, haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu kwa kuzingatia usawa wa kijinsia,"amesisitiza.
Rais Mwinyi amesema changamoto na majanga mbalimbali ambayo bara la Afrika linapitia, waathirika wake wakubwa ni wanawake na watoto na kutambua hilo Tanzania imeendelea kuchukua hatua katika kutatua migogoro mbalimbali.
"Kwa mfano hivi sasa Tanzania inashiriki katika Jeshi la Umoja wa Mataifa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Stabilization Mission) na jeshi la kulinda amani na katika kuepusha uvunjifu wa haki za binadamu unaotokana na vita, kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania inashiriki katika jeshi la pamoja la kulinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo," amesema.