Rais Mwinyi: Ipo haja kuongeza huduma, wataalamu wa figo

Muktasari:

  • Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema pamoja na Tanzania kupiga hatua za matibabu ya ugonjwa wa figo ikiwa ni pamoja na kuwa na vituo 260 vya kusafisha damu, ipo haja ya kuongeza huduma na wataalamu wenye uwezo kuleta ufanisi zaidi.

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema pamoja na Tanzania kupiga hatua za matibabu ya ugonjwa wa figo ikiwa ni pamoja na kuwa na vituo 260 vya kusafisha damu, ipo haja ya kuongeza huduma na wataalamu wenye uwezo kuleta ufanisi zaidi.

 Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 24, 2022 wakati akifungua kongamano la nane la Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Figo (NESOT) mjini Unguja, ambapo amesema jambo la faraja ni madaktari bingwa wa figo 38 ikilinganishwa na madaktari wanne waliokuwapo wakati chama kinaanzishwa mwaka 2012.

“Hata hivyo kutokana na idadi ya Watanzania (milioni 61.7) na kuendelea kuongezeka kwa magonjwa ya figo ikilinganishwa na mahitaji, ipo haja ya kuwa na wataalamu wengi zaidi,” amesema

Amesema takwimu za Tanzania zinaonyesha watu saba hadi 10 kati ya watu 100 wana tatizo la figo “takwimu hizi tunapata picha kuwa tatizo la figo ni kubwa.”

Amesema Serikali zote mbili, zinatambua changamoto zinazowakumba wataalmu hao hivyo zipo tayari kutoa msaada wowte kukabiliana nazo.

Amesema ili kuongeza ufanisi na kukabiliana na changamoto hizo, aliwataka viongozi wa NESOT, kuwaelekeza wanachama wake wawe mfano bora kuwavutia vijana wapya wahamasike kusomea na kujiunga katika tiba hiyo huku chama kikiwajengea uwezo wataalamu kuanzia hospitali za rufaa hadi huduma za msingi.

Pia amewataka kuzingatia namna bora ya kuwaelimisha watanzania kujikinga na magonjwa haya ambapo ni pamoja na kuzingatia lishe bora, kupungua matumizi ya chunvi na mafuta, uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe na kuhimizana umuhimu wa kufanya mazoezi.

Naye Mwenyekiti wa NESOT, Dk Onesmo Kisanga amesema utafiti uliofanyika dunia nzima asilimia 10 ya wagonjwa wanamagonjwa ya figo.

Kwa Tanzania ngazi ya jamii takwimu zinaonyesha asilimia 6.7 (ya watu 61.7 milioni) wana magonjwa ya figo na kiasi kikubwa inachangiwa na uelewa mdogo wa jamii kuhusu ugonjwa huo.

Amesema tatizo la figo linakuwa kubwa kutokana na magonjwa yasiyoambukiza kuongezeka ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa katika ugonjwa huo hivyo kutaka ushirikiano wa kutoa elimu kwa jamii.

Naye Daktari Bingwa wa figo na mkuu wa kitengo cha usafishaji damu Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar, Maryam Hamad amesema Zanzibar kuna mashine 10 za kusafisha damu na wagonjwa 45 wanasafishwa kila wiki huku huduma hiyo ikitolewa bure.

Amesema vyanzo vikuu vya ugonjwa wa figo ni maradhi ya sukari na shinikizo la damu huku vyanzo vingine ni mashambulizi ya bakteria, kupungua maji mwilini hata wakati wa ajali kwahiyo wananchi wanashauriwa kupunguza kutumia vyakula vinavyosababisha magonjwa hao.

Waziri wa Afya Zanzibar, Ahmed Mazrui amesema kwa utafiti usio rasmi, vijana wengi wenye umri chini ya miaka 20 wanaathiriwa na figo huku chanzo kikubwa ni matumizi ya vinywaji vikali na kuwataka wataalmu hao kufanya utafiti zaidi kubaini ukweli huo.

Katika kongamano hilo la siku mbili, wapo watalaamu kutoka Ujerumani, UK, Afrika kusini na Kenya watakaotoa mada mbalimbali.