Rais Samia afanya mabadiliko madogo Baraza la Mawaziri


Muktasari:

  • Katika kuendelea kuwa na wizara zilizo imara, Rais Samia ameendelea kupangua mawaziri wake baada ya kuwapishanisha ofisi Waziri, Jenista Mhagama kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) na George Simbachawene Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri akiteua mawaziri wawili Jenista Mhagama kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) na George Simbachawene kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

 Awali kabla ya uteuzi huo Simbachawene alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) ambapo nafasi hiyo imechukuliwa Jenista Mhagama.

Simbachawene amekuwa akiguswa na mabadiliko yanayofanywa na Rais tangu wakati wa Serikali ya awamu ya tano ya hayati John Magufuli, na wakati wote amekuwa akivuka salama wakati wengine wakiachwa.

Rais Samia alipofanya mabadiliko ya Baraza lake la Mawaziri baada ya kuapishwa, alimbakisha Simbachawene katika Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo aliteuliwa na hayati Magufuli Desemba 5, 2020.

Hata hivyo, Januari 8 mwaka 2022, Rais Samia alifanya mabadiliko madogo ya mawaziri na kumhamisha waziri huyo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda Wizara ya Katiba na Sheria, akichukua nafasi ya Profesa Palamagamba Kabudi.

Waziri Mhagama anachukua nafasi ya Simbachawene ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Uteuzi huu umeanza leo Aprili, Mosi 2023 huku mawaziri wateule wakiapishwa kesho Aprili 2, 2023 Ikulu, Dar es Salaam.