Samia aachia mkeka mwingine, ateua, apangua mawaziri

What you need to know:

  • Katika uteuzi huo, Rais Samia amewateua pia amewapangua manaibu katibu wakuu na amemteua mkuu wa mkoa mmoja na Kamshna wa Tume ya Uchaguzi

Dar es Salaam. Ni mkeka mpya tena. Unaweza kusema hivyo. Hii ni kutokana na kupita siku chache tangu Rais Samia Suluhu Hassan afanye mabadiliko madogo katika baraza lake la Mawaziri na leo tena amefanya mabadiliko mengine.

Februari 14, Rais Samia alifanya mabadiliko madogo ya kuteua aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na Balozi Dk Pindi Chana aliyekuwa Maliasili na Utalii kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Rais pia alifanya mabadiliko ya makatibu wakuu wawili, alimteua Dk Hassan Abbas kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Said Yakub kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo.

Leo Rais Samia ametoa mkeka mwingine wenye orodha mpya ya wateule katika nafasi za mawaziri, naibu mawaziri, na katibu wakuu, naibu makatibu wakuu na wakuu wa mikoa.

Mkeka wa leo umehusisha pia uteuzi wa Mkurugenzi mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhani Kailima akichukua nafasi ya Dk Wilson Mahera aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)-Afya.

Hii ni mara ya pili kwa Kailima kushika wadhifa huo, mara ya kwanza aliteuliwa Julai 25, 2015 na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, mkeka huo umehitimisha wadhifa wa Mashimba Ndaki kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na nafasi hiyo imechukuliwa na aliyekuwa Naibu wake, Abdallah Ulega.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Februari 26, 2023 na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka, pamoja na Ulega, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Katika taarifa hiyo, Pauline Gekul amehamishwa kutoka Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo kwenda Wizara ya Katiba na Sheria akichukua nafasi ya Geofrey Pinda.

Pinda amehamishwa kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akichukua nafasi ya Ridhiwani Kikwete aliyehamishiwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wadhifa aliokuwa nao Deogratius Ndejembi.
Ndejembi sasa anakuwa Naibu Waziri wa Tamisemi kumrithi David Silinde aliyehamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Katika uteuzi huo, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, Christina Mndeme ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, akichukua nafasi ya Sophia Mjema aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Itikadi na Uenezi.

Dk Francis Michael naye amehamishwa kutoka Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe akichukua nafasi ya Waziri Kindamba aliyehamishiwa Tanga.

Mabadiliko hayo yamemtupa nje, Omary Mgumba aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dk Tausi Kida ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Uwekezaji, Juma Mkomi anaushika wadhifa huo katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora.

Balozi Samwel Shelukindo naye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, huku Profesa Carolyne Nombo akiukwaa ukatibu mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Gerald Mweli anakuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Seif Shekalage anaushika wadhifa huo katika Wizara ya Afya na Nadhifa Kemikimba, anakuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maji.

Kheri Mahimbali anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Madini na Mohammed Khamis anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akichukua nafasi ya Dk. Jim Yonazi aliyehamishiwa Ofisi ya Rais Sera, Bunge na Uratibu.
Kulingana na taarifa ya Ikulu, Makatibu Wakuu kadhaa wamehamishwa wizara akiwemo Profesa Rizik Shemdoe kutoka Tamisemi hadi Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mwingine ni Dk John Jingu aliyehamishwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu hadi Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wanawake na Makundi Maalum.

Adolf Ndunguru amehamishiwa Wizara ya Tamisemi akitokea Wizara ya Madini na Anthon Sanga amehamishiwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutoka Wizara ya Maji.

Kwa upande wa Naibu Makatibu Wakuu wapya ni Sospeter Mtwale aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, akitoka kuwa Ofisa Mwandamizi Ofisi ya Rais Ikulu.

Mwingine ni Dk Franklin Rwezimula aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia akitokea kuwa Meneja wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kati.

Kadhalika, Dk Hussein Omar ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, kabla alikuwa Ofisa Mwandamizi Ofisi bya Makamu wa Rais.