Rais Samia afichua siri uteuzi wa Makonda RC Arusha

Muktasari:

  • Asema anaamini Makonda atafanya kile anachotamani akafanye mkoani Arusha.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amemweleza Paul Makonda kuwa utendaji wake ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, akautumie Arusha kuufanya uwe mkoa mzuri.

 Amesema miezi mitano aliyohudumu katika nafasi ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo ndani ya CCM amesaidia kukichangamsha chama hicho na kuwafanya wengine wafanye kazi zao.

Rais Samia amesema hayo leo Aprili 4, 2024, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa halfa ya kuwaapisha viongozi aliowateua katika nafasi mbalimbali, akiwamo Makonda.

“Paul umefanya kazi nzuri CCM, umekichemsha chama kulikuwa kidogo na uvivu kila mmoja kutoka hataki kuna waliosinzia, lakini umeingia njiani umekichemsha chama tumeamka vizuri, lakini najua ulikuwa RC Dar es Salaam na kwenyewe ulifanya mazuri,” amesema na kuongeza:

“Tumekupeleka Arusha, unajua nini kipo huko na unajua nini matumaini yangu kwako huko Arusha. Nenda kafanye kazi, mimi nina imani kubwa nawe na ninaamini utafanya kile ninachotamani ukafanye.”

Rais Samia amesema, “Kubwa Arusha ni utalii, wageni wameongezeka, malazi hakuna kwa hiyo nenda kasimamie ukisaidiana na wawekezaji kuhakikisha tunapata malazi ya kutosha kwa ajili ya wageni wetu.”

“Arusha pia ni mji mkubwa, ni makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na taasisi kubwa zipo kule kwa hiyo nenda kasimamie mkoa uwe na jina zuri,” amesema.