Rais Samia ajadili mwenendo wa uchaguzi CCM

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu HassanĀ  akizungumza na kamati ya siasa ya chama hicho Mkoa wa Tabora (hawako pichani) leo Jumatano Mei 18, 2022.

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na kamati ya siasa ya Mkoa wa Tabora.

Tabora. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na kamati ya siasa ya Mkoa wa Tabora.

Pia, Rais Samia amepokea taarifa ya mwenendo wa uchaguzi wa ndani ya chama hicho unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka imesema Rais Samia amekutana na kamati hiyo leo Jumatano Mei 18, 2022 kwenye ofisi za Chama mkoani humo.

Imesema kuwa pamoja na mambo mengine, Rais Samia amepokea taarifa ya mwenendo wa uchaguzi na kujadiliana masuala mbalimbali kwa ustawi na chama mkoani humo.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Hassan Mwakasubi amemweleza Rais Samia kuwa Chama na wananchi wa mkoa huo wanaridhishwa na utendaji wa Serikali katika kuimarisha utoaji huduma za kijamii, ujenzi wa miundombinu na ukuzaji wa uchumi.

"Nimekuwa mwanachama wa chama hiki na kiongozi kwa miaka 25, lakini tukio la Rais Samia kutembelea ofisi zetu na kuzungumza na viongozi wake hili ni tukio la kwanza hapa kwetu. Haya ni mahusiano mazuri baina ya chama na Serikali, tunakushukuru sana na tunakukaribisha Tabora," amesema Mwakasubi.

Rais Samia yupo mkoani hapa kwa ziara ya siku tatu aliyoianza Mei 17, 2022 na atahitimisha kesho Mei 19, 2022 kwa kuwahutubia wananchi kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.