Rais Samia amlilia Lowassa

Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan amlilia Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akisema Taifa limepoteza kiongozi mahiri aliyejituma na kujitoa kwa ajili ya nchi.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akisema Taifa limepoteza kiongozi mahiri na shupavu.
Kifo cha Lowassa kimetangazwa leo Februari 10, 2024 na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ambaye amesema kiongozi huyo amefariki dunia akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Dk Mpango, Lowassa alikuwa akisumbuliwa na maradhi matatu ambayo ni kujikunja kwa utumbo, shinikizo la damu na mapafu.
Lowassa aliyehudumu katika nafasi ya Waziri Mkuu kwa miaka mitatu kati ya mwaka 2005 hadi 2008 amefariki dunia leo Februari 10, 2024 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Katika salama zake za rambirambi alizotoa kupitia ukurasa wake wa X, Rais Samia amemtaja Lowassa kama kiongozi mahiri aliyejituma na kujitoa kwa ajili ya Tanzania.
“Lowassa ameitumikia nchi yetu katika nafasi mbalimbali kwa zaidi ya miaka 35, akianzia ushiriki wake katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), mbunge, waziri katika wizara mbalimbali na waziri mkuu.”
“Tumempoteza kiongozi mahiri, aliyejituma na kujitoa kwa nchi yetu. Natoa pole kwa mjane, Mama Regina Lowassa, watoto, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mzito,”ameandika Rais Samia.
Rais Samia ameendelea kusema: “Katika mawasiliano yangu na familia, nimewaeleza kuwa kama Taifa tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu, na kamwe wasiache kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutafakari neno lake, hasa Kitabu cha Ayubu 1:21.”