Rais Samia ashtukia mchezo mchafu mfumo haki jinai, aunda tume

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali kabla ya kuzindua Tume ya kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma  leo Januari 31, 2023. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Kutokana na malalamiko ya wananchi kwa taasisi zinazosimamia mfumo wa haki jinai ikiwamo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Jeshi la Polisi, Magereza na Mahakama, Rais Samia Suluhu Hassan ameunda tume kuchunguza malalamiko hayo.

Mwanza. Wakati Taifa likisubiria ripoti ya matumizi ya fedha zaidi ya Sh50 bilioni zilizotokana na makubaliano ya washtakiwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Rais Samia Suluhu Hassan amesema ofisi hiyo ilipitia kipindi ambacho kuna michezo ilikuwa inafanyika ambayo iliharibu taswira ya taasisi hiyo.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowashirishwa bungeni Aprili, 2021 iliainisha kuwepo kwa bakaa ya fedha zaidi ya Sh50 bilioni zilizotokana na mali zilizotaifishwa na kurejeshwa serikalini chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali (DPP) hadi kufikia Juni 30, 2020 kupitia kesi zilizomalizika kwa kipindi cha miaka sita.

Oktoba 14, 2022, CAG Charles Kichere alisema ifikapo Machi, 2023 watamkabidhi Rais Samia ripoti ya matumizi ya fedha hizo zilizotokana na makubaliano ya washtakiwa na DPP, ambapo sasa maofisa wake wanawahoji watu waliotajwa kuhusika na sakata hilo kuanzia ngazi ya kata.

Akizungumza leo Jumanne Januari 31, 2023 Ikulu Chamwino, Dodoma wakati akizindua tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini, Rais Samia ameitaka tume hiyo kuichunguza ofisi hiyo juu ya utendaji kazi na uendeshaji ili kubaini kasoro zilizopo na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuiboresha iweze kutoa haki kwa wananchi.

Amesema mbali na ofisi hiyo ya mashtaka tume hiyo itakayoanza kazi kesho Jumatano hadi Mei 30 itazifanyia tathmini taasisi za utoaji haki jinai nchini ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na kuibua manung’uniko kwa wananchi, ikiwamo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Jeshi la Polisi, Magereza na Mahakama.

“Kutokana na ukubwa wa kazi tunawapa miezi minne kuanzia kesho hadi Mei 30 nendeni mkaangalie Ofisi ya Mashtaka kwenyewe kukoje na kuna kasoro zipi.

“Zamani ofisi hii kulikuwa na ngoma nzito inachezwa mpaka kukusanya fedha za plea bargaining nyingine zimeonekana na nyingine hazijaonekana ukifuatilia utaambiwa mara kuna akaunti China.

“Tutazame kuna nini haswa kilichoharibu hii taasisi, pia tuiangalie Takukuru kwa sababu kubadilisha tu mkuu wa taasisi haisaidii watamdanganya tu wafanye wanavyotaka.

“Jeshi la Magereza na kwenyewe tukalitazame, magereza zetu zikoje na zinatakiwa ziweje, mwendelezo wake na kama linafanya kazi ya msingi? Mamlaka ya Kuzuia Dawa za Kulevya nako kuna changamoto nyingi za kutegea watu dawa,” amesema Rais Samia.

Naye, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amempongeza Rais kwa kuanzisha tume hiyo ili Watanzania waweze kupata haki kwani kumekuwa na manung’uniko mengi ya wananchi juu ya mfumo wa utoaji haki jinai nchini.