Rais Samia ataka utekelezaji sera, mikakati kuboresha kilimo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali, Maspika, Naibu Maspika pamoja na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 53 wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF) uliofanyika jijini Arusha Julai 3, 2023. Picha na Ikulu
Muktasari:
- Ni wakati wa nchi za SADC kuanza kutekeleza mipango na mikakati iliyojiwekea katika kuimarisha sekta ya kilimo.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema licha ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kujiwekea mikakati na sera za kuboresha sekta ya kilimo, bado zinatajwa kuwa na njaa.
Amesema ni wakati sasa nchi hizo zitumie mikakati na sera hizo ili kuufanya ukanda wa SADC kuwa mzalishaji na msambazaji mkubwa wa chakula Afrika na kwingineko.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Julai 3, 2023 katika mkutano wa 53 wa Jumuiya ya Wabunge wa nchi za SADC uliofanyika jijini Arusha.
Kulingana na mkuu huyo wa nchi aliyealikwa kuwa mgeni rasmi, nchi za SADC zina kilometa za mraba milioni 9.85 zinazofaa kwa shughuli ya kilimo.
“Kama zitatumiwa vyema, tuna ardhi muhimu kwa ajili ya kilimo lakini tunapaswa kuhakikisha ardhi hii inazalisha chakula kuziba pengo linalofanya nchi za SADC kuwa na njaa,” amesema.
Namna njema ya kufanikisha hilo, amesema ni utekelezaji wa sera mbalimbali na mikakati inayowekwa mara kwa mara kama ule wa mwaka 2015 wa SADC.
“Tunakuja na sera na mikakati mbalimbali lakini hatutekelezi, sasa huu ni wakati wa kuzungumza na kuanza kutekeleza,” amesema.
Ili kukabiliana na changamoto mbalimbali, amesema mabunge ya nchi wanachama yana kazi kubwa ya kufanya kubadilisha sera mbalimbali za kilimo.
Kuhusu usawa wa jinsia, amewataka viongozi wote kuendelea na jitihada na kupaza sauti zao kuhakikisha haki inatendeka.
“Tumejitambulisha katika ulingo mwaka 1995 na mengi yamebadilika, bila hayo Rais Samia asingesimama hapa leo kama Rais wa Tanzania,” amesema.