Rais Samia ataka wakuu wa mikoa kuwatafutia maeneo ya biashara wamachinga

Rais Samia ataka wakuu wa mikoa kuwatafutia maeneo ya biashara wamachinga

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa mikoa nchini kuwapanga wamachinga katika maeneo stahiki bila kusababisha vurugu.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa mikoa nchini kuwapanga wamachinga katika maeneo stahiki bila kusababisha vurugu.

Akizungumza leo Septemba 13 Ikuli ya Chamwino mkoani Dodoma wakati wa kuwaapisha viongozi aliowateua jana, Rais Samia amesema licha ya serikali kutoa fursa kufanya biashara kama njia ya ajira kwao, wamekuwa wakifanya kazi katika maeno tofauti na wakati mwingine kuziba maduka ya watu.

"Watu hawa sasa wameenea kila mahali, hadi kwenye maduka wanaziba, wenye maduka hawauzi wanauza wao mbele hadi wenye maduka baadhi yao wamepata mtindo wa kutoa bidhaa ndani na kuwapa machinga kuwauzia kwa sababu watu hawangii ndani," amesema Samia.

Amesema kitendo hicho kinawakosesha kodi kwa sababu wafanyabiashara hao hawalipi lakini mwenye duka anatakiwa kulipa kodi.

"Wakuu wa mikoa ninawaagiza kuchukua hatua za kuwapanga vyema, ninaposema kuchukua hatua za kuwapanga vyema sitaki kuona yale ninayoyaona kwenye TV, ngumi kupigana, kuchafuliana, vitu kumwagwa hapana, mmaweza kuchukua hatua vizuri na kuwpaanga vyama bila kiudhi wenye maduka, wamachinga na maisha hakaendelea," amesema.

Amewataka kuhakikisha kuwa wanapochukua hatua hizo wasisababishe vurugu, fujo wala uonevu.

"Wito wangu pia kwa  ndugu zetu wamachinga na wajasiramali, wajitahidi kufuata sheria na kanuni zilizopo, wajitahidi pia kufuata yale wanayopangiwa na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya," amesema Samia.