Rais Samia: Tuendako Serikali itaendeshwa kwa matendo makali

Rais Samia: Tuendako Serikali itaendeshwa kwa matendo makali

Muktasari:

  • Rais Samia amesema katika kipindi cha miezi sita ya urais wake amekuwa mtulivu na mkimya, akisoma Wizara zote zinavyoendeshwa, lakini kuanzia sasa ataendesha Serikali yake kwa vitendo.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema katika kipindi cha miezi sita ya urais wake amekuwa mtulivu na mkimya, akisoma Wizara zote zinavyoendeshwa, lakini kuanzia sasa ataendesha Serikali yake kwa vitendo.

Akizungumza leo Septemba 13 wakati wa kuwapisha viongozi aliowateua, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, Rais Samia amesema katika kipindi hicho watendaji wake walimsoma pia, huku akibainisha kuwa kati yao walichukulia ukimya wake kama udhaifu na kuanza kufanya yanayowapendeza.

Amesema wengine walichukulia ukimya na utulivu wake kama njia ya wao kufanya kazi na kuonyesha kuwa wanaweza kufanya kazi.

"Nataka niwaambie, kipindi cha miezi sita nilikuwa najifunza, nilikuwa Makamu wa Rais nilikuwa na ninyi lakini sikuwa na fursa ya ndani ya kujifunza utendaji wa ndani wa Wizara hivyo nilikuwa najifunza na nimeona sasa vipi nakwenda na nyie," amesema Samia.

Amesema katika uongozi kuna mbinu nyingi na yeye amejichagulia njia yake.

"Nataka niwaambie kwamba, tunapoendelea huko, Serikali yetu itaendeshwa kwa matendo makali na siyo maneno makali. Ninaposema matendo makali siyo kupigana mijeredi ni kwenda kwa Wananchi na kutoa huduma inayotakiwa kila mtu kufanya wajibu wake.

"Msinitegemee kwa maumbile yangu haya pengine na malezi yangu kukaa hapa nianze kufoka. Nahisi si heshima, kwa sababu nafanya kazi na watu wazima wanaojua jema na baya ni lipi kwahiyo ni imani yangu kuwa tunapozungumza tunaelewana na kila mtu anajua afanye nini kwenye majukumu yake. Sitafoka kwa maneno, nitafoka kwa kalamu," amesema Samia.

Amesema kipindi hicho cha kiezi sita kuna watu waliichukulia poa serikali ya wamu ya sita na kufanya wanayotaka.

"Adjustment (mabaddiliko) hizi zinaendelea, tutakavyoendelea wizara hii nayo tutaifanyia marekebisho nao watakuja kuapa mbele yenu. Niseme tu mabadiliko haya matengenezo haya kutokana na jinsi nilivyoona utendaji wa mawaziri wangu na watendaji wengine kwenye mawizara bado yatakuwa yanaendela," amesema Samia.