Rais Samia atengua watano akiwemo DC Mbarali

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amewatengua Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune na Wakurugenzi wa halmashauri wanne.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametengua nafasi za watendaji watano akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Mbarali (DC), Reuben Mfune anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Zuhura Yunus leo Jumanne, Januari 24, 2023, inawataja mwingine aliyetenguliwa ni Msongela Palela Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Musoma (DED), Mkoa wa Mara.

Wakurugenzi wengine wa halmashauri waliotenguliwa kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Michael Matomora wa Iramba, Linno Pius wa Ushetu na Sunday Ndori wa Halmashauri ya Ludewa.

Januari 11, 2023, Mfune alifikishwa mahakamani akituhumiwa katika kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh51 milioni.