Rais Samia ateua viongozi Tume ya Walimu, TADB na TCB

Profesa Masoud Muruke.

Muktasari:

  1. Taarifa ya uteuzi wa Profesa Muruke imetolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, aliyeko Paris, nchini Ufaransa kwenye ziara ya Rais Samia.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemteua Profesa Masoud Muruke kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), akichukua nafasi ya Profesa Willy Komba aliyemaliza muda wake.

Profesa Komba ameiongoza TSC tangu Juni 2020 na wadhifa wake umekoma leo Jumatano, Mei 15, 2024, baada ya muda wake wa utumishi ndani ya TSC kumalizika.

Taarifa ya uteuzi wa Profesa Muruke imetolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, aliyeko Paris, nchini Ufaransa kwenye ziara ya Rais Samia.

Rais Samia yupo Ufaransa kushiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Afrika uliofanyika nchini humo, jana Jumanne, Mei 14, 2024.

Katika uteuzi huo, wengine walioteuliwa kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Ishmael Kasekwa anayeenda kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Kasekwa ameteuliwa kushika wadhifa huo kwa kipindi cha pili, baada ya kumaliza muda wake wa awali.

Sambamba na hao, Rais Samia pia amemteua Balozi Maimuna Tarishi kuwa mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.

Balozi Tarishi anarithi mikoba kutoka kwa Profesa Joseph Bucheishaija aliyemaliza muda wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, Rais Samia pia amemteua Martin Kilimba kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Biashara Tanzania (TCB).

Kilimba anaenda kuchukua nafasi ya Dk Edmund Mndolwa, mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi, ambaye muda wake umemalizika.