Rais Samia awapa ujumbe mawakili EAC

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati akifungua mkutano wa 22 wachama cha Mawakili wa Afrika ya Mashariki (EALS), jijini Arusha.

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassana amefungua mkutano wa 22 wachama cha Mawakili wa Afrika ya Mashariki (EALS), jijini Arusha. Pamoja na mambo mengine, mkutano huo utachagua viongozi wao watakaoongoza kwa kipindi cha miaka miwili.

Arusha. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Mawakili wa Afrika ya Mashariki kuwa wazalendo kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kwa kuhakikisha wanalinda amani na utulivu kutokana na kutetea haki.

Amesema hayo leo Alhamisi, Novemba 24, 2022 wakati akifungua mkutano wa 22 wachama cha Mawakili wa Afrika ya Mashariki (EALS), jijini Arusha.

Rais Samia amesema lengo la EAC ni kuwaunganisha wananchi, kuleta amani, utulivu na kusaidia kukuza uchumi.

"Tufanyekazi kwa ushirikiano, tujenge mazingira ya kuaminiana ili tuwe na ushirikiano thabiti," amesema

Pia, Rais Samia amewataka mawakili hao kuhakikisha wanasimamia haki katika utekelezaji wa kazi zao ili kuhakikisha amani na utulivu vinadumu katika Afrika ya Mashariki.

Katika mkutano huo, Rais Samia amewataka mawakili hao kujifunza wimbo wa Afrika ya Mashariki kwani amebaini wengi walishindwa kuimba.

"Ili mjisikie wote Wanaafrika ya Mashariki, mkariri na kuimba wimbo ya Afrika ya Mashariki, mfano sisi Waslamu tunaamini Mungu ni mmoja na Mtume Mohamad ni mjumbe wake, karibu kila siku katika swala tunamtaja zaidi mara tano hii inakupa kuamini zaidi," amesema

Katika mkutano huo, Rais Samia amewataka mawakili kusimama pamoja kama Waafrika wa Afrika ya Mashariki hasa katika kukabiliana na changamoto za utandawazi, teknolojia na masuala ya ikolojia kwa kufanya kazi kwa pamoja lakini kwa kuzingatia historia, tamaduni na desturi za kila nchi.

Rais Samia amekubali maombi ya chama hicho kupatiwa ardhi ya ujenzi wa makao makuu lakini pia kurahisisha ufanyaji wa kazi kwa ushirikiano baina ya mawakili wa nchi wanachama.

Awali, Rais wa EALS, Bernard Oundo ameomba kuboresha mazingira ya mawakili kufanyakazi ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo, kupata ardhi ya ujenzi wa makao makuu.

Katika mkutano huo ambao unaendelea jijini Arusha, chama hicho kitachagua viongozi wake akiwepo Rais mpya ambaye anaongoza kwa miaka miwili.