Rais Samia: Bidhaa zote zitapanda bei

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema bidhaa zote nchini zitapanda bei kutokana na athari ya vita ya Russia na Ukraine.

Zanzibar. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema bidhaa zote nchini zitapanda bei kutokana na athari ya vita ya Russia na Ukraine.

 Amesema kuwa mabadiliko ya kupanda bei za bidhaa yanatatokana na kupanda bei ya mafuta duniani ambazo zinaithiri pia Tanzania.

Rais Samia ametoa tahadhari hiyo leo Jumanne Machi 8, 2022 wakati wa maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika katika viwanja vya Maisara, Zanzibar.

Ametoa tahadhari hiyo ikiwa zimepita siku 10 tangu Serikali itangaze kuondoa tozo katika kila lita ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Februari 28, 2022 Serikali kupitia Wizara ya Nishati ilitangaza kuondoa tozo ya Sh100 kwa kila lita ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa miezi mitatu kuanzia mwezi Machi.

Wizara hiyo ilisema kuwa sababu za kuondoa tozo hiyo ni kutokana na kuendelea kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia kunakosababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo vita kati ya Russia na Ukraine.

Leo, Mkuu huyo wa nchi amesema kuwa kutakuwa na mabadiliko ya kupanda kwa bei za bidhaa zote nchini ambayo yamechagizwa na vita hiyo.

“Eneo la pili la mabadiliko haya ambalo kidogo limechagizwa na uwepo wa vita hii ya Ukraine na Russia ni kupanda kwa bei za mafuta, mafuta yanapanda bei mno na jinsi mafuta yanavyopanda bei Tanzania hatutonusurika, bidhaa zote zitapanda bei, nauli zote zitapanda bei, kila kitu kitapanda bei” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Thamani ya kila kitu itapanda kwa sababu mafuta yanapanda bei”

Amesema kuwa kupanda kwa bidhaa hakusababishwi na viongozi kama ambavyo baadhi wanavyodai

“Tumeanza kusikia minong’ono kuwa maisha yanapanda bei, kila kitu kinapanda bei, ni hawa viongozi wetu hawana baraka, hili sio Baraka ya kiongozi ni hali ya ulimwengu inavyokenda

“Mafuta yanapanda bei duniani na bidhaa zote zitapanda bei” amesisitiza Rais Samia

Maadhimisho hayo yanayofanyika visiwani Zanzibar yamehudhuriwa na Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, mawaziri, baadhi ya mabalozi na wawakilishi wa mashirika mbalimbali, pamoja na viongozi wa baadhi ya vyama vya siasa.