Rais Samia kufanya ziara ya siku tano nchini Uturuki

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, January Makamba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Rais Samia anatarajia kufanya ziara nchini Uturuki kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdoğan ikiwa ni miaka 14 tangu Rais wa Tanzania alipokwenda katika ziara ya kiserikali.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku tano nchini Uturuki kati ya Aprili 17 hadi 21, 2024 kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdoğan.

Samia anakwenda ziara hiyo ikiwa ni miaka 14 imepita tangu Rais wa Tanzania alipotembelea nchi hiyo ikiwa ni miaka saba tangu Rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdogan alipotembelea Tanzania, Januari 2017.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Aprili 15, 2024 juu ya ziara hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, January Makamba amesema Uturuki ni kati ya nchi zilizoweka msisitizo katika mahusiano yake  na nchi za Afrika, jambo lililojenga muingiliano wa watu kati ya nchi hizi mbili.

“Wafanyabiashara wengi wa Tanzania wamekuwa wakienda kukununua bidhaa Uturuki na sisi tumekuwa tukiuza bidhaa nyingi huko, i hivyo lengo la kwanza ni kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, kibiashara na kisiasa kati ya nchi hizi mbili,” amesema Makamba.

Makamba amesema lengo la ziara hiyo pia ni kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kiuchumi kwani Tanzania inahitaji mitaji, teknolojia na wawekezaji.
“Tumeona kampuni nyingi kutoka Uturuki zinafanya kazi hapa nchini, Uturuki ni miongoni mwa nchi 20 zilizo na uchumi mkubwa duniani, hivyo kuwa nayo karibu tutanufaika kibishara na kiuwekezaji,” amesema Makamba.

Ushirikiano katika maendeleo pia ni moja ya jambo ambalo linaangaziwa, kwani nchi hiyo imekuwa ikiisaidia Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo maji, afya na elimu.

Makamba amesema mbali na Rais kufanya mazungumzo ya kiserikali na mwenyeji wake kupitia maeneo ya ushirikiano yaliyopo, pia yataangazia maeneo mapya ambayo yanaweza kutumiwa kati ya nchi hizo mbili.

“Baada ya kumaliza mazungumzo hayo, Rais Samia atakwenda mjini Instanbul ambao ndiyo mji wa kibiashara na huko limeandaliwa kongamano kubwa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki, ambalo litakutanisha wafanyabiashara wa pande zote,” amesema Makamba.

Baada ya kongamano hilo, Rais atakutana na kampuni kubwa 15 nchini humo kwa ajili ya kuwashawishi kuja kuchangamkia fursa zilizopo Tanzania.

“Kuna maeneo ambayo tunashirikiana nao yalitarajiwa kuwa maeneo zaidi ya 10 lakini hadi sasa tuna maeneo kama sita,  ambayo yamethibitishwa kuwa tutasainiana mikataba na hati za makubaliano,” amesema Makamba.

Miongoni mwa maeneo ambayo wanatarajia kuingia makubaliano Tanzania na Uturuki ni ufadhili wa masomo ya elimu ya juu.