Rais Samia kufanya ziara Mtwara, ni baada ya tangazo la kuwafuta kazi DC, DED

Muktasari:

  • Siku chache baada ya kutangaza kumfukuza kazi Hanafi Msabaha, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, pamoja na Tatu Issike, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya siku nne mkoani hapa.

Mtwara. Siku chache baada ya kutangaza kumfukuza kazi Hanafi Msabaha, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, pamoja na Tatu Issike, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya siku nne mkoani hapa.

Akizungumza kwenye kikao kazi cha wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa yote nchini mwezi Agosti, Rais Samia alitangaza kuwa atamfukuza kazi viongozi hao, kutokana na kushindwa kusimamia majukumu yao ikiwemo wananchi kurudisha kadi za Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wananchi wa Kata ya Muungano Kijiji cha Lyowa Wilaya ya Mtwara walitangaza kurudisha kadi za CCM baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa viongozi hao kubadilisha matumizi fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari ya Kata ya Muungano.

Hata hivyo, awali DC alisema wananchi walifikia maamuzi ya kujenga Sekondari katika Kijiji mama cha Muungano kwenye kikao kutokana na kata hiyo kutokuwa na shule ya sekondari.

Akizungumzia ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanal Ahmed Abbas, amesema kuwa Rais Samia anatarajia kufanya ziara hiyo kuanzia Sept 14-17 mwaka huu.

Amesema kuwa katika ziara hiyo Rais anatarajia kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa ilani ya CCM, pamoja na kukagua miradi ya maendeleo na kuangalia utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wakuu wa serikali na chama yaliyotolewa katika nyakati tofauti  katika mkoa wa Mtwara.

“Kutokana na heshima hiyo naomba mjitokeze kwa wingi kumlaki katika maeneo yote atakayopita na kujitokeza katika mikutano na miradi yote atakayotembelea”

“Ili mpate taarifa kamili tutaendelea kutoa taarifa na ratiba kamili ya matukio yatayojiri katika ziara hiyo ya kiongozi mkubwa wa nchi” amesema Kanal Abbas