Rais Samia kuhusu uteuzi wa Dk Tax kwenda Wizara ya Ulinzi

Rais kuhusu uteuzi wa Dk Tax kwenda Wizara ya Ulinzi

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amesema katika mabadiliko aliyofanya ameamua kuvunja ile dhana ya muda mrefu kuwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa lazima akae mwanaume mwenye misuli yake huku akibainisha kuwa kazi ya waziri katika wizara hiyo si kupiga mzinga wala kubeba bunduki.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema katika mabadiliko aliyofanya ameamua kuvunja ile dhana ya muda mrefu kuwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa lazima akae mwanaume mwenye misuli yake huku akibainisha kuwa kazi ya waziri katika wizara hiyo si kupiga mzinga wala kubeba bunduki.


Badala yake, waziri ni msimamizi wa sera na utawala wa wizara husika ndiyo maana aliamua kumpeleka Dk Stergomena Tax.
Amesena hayo ikiwa ni muda mchache baada ya kuwaapisha mawaziri wanne aliowateua na Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hafla niliyofanyika Ikulu, Chamwino jijini Dodoma.


"Nimempeleka huko si tu kwa sababu tu kuvunja mila bali kwa upeo wake mkubwa ambao aliupata akiwa SADC, kipindi chote tukienda SADC alikuwa anasimamia vyema mambo yote ya usalama ndani ya ukanda alikuwa na upeo mkubwa katika maeneo ya nchi za Afrika ya Mashariki,"


"Kwa uzoefu alioupata hasa katika sekta ya ulinzi kikanda atakwenda kutusaidia huko, yeye anajua vyema askari wetu waliopo Mozambique, waliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kwanini wako huko, mifumo yao wanavyobadilika haki zao nahisi atamsaidia vizuri CDF katika Upande huo."


Amesema ni natumaini yake kuwa aliowateua watafanya kazi vizuri huku akibainisha kuwa kuteuliwa kwao hakumaanishi kuwa wao ni bora kuliko wengine.


"Uzuri wenu utaonekana katika utekelezaji wa majukumu yenu kwani hata tuliowachagua mwanzo walikuwa wazuri pia, hivyo mtakavyotekeleza vizuri ndivyo uzuri wenu utaweza kuonekana,"


"Kwangu mimi ninachotaka kuona ni matokeo, sitaki kuwaona kwenye TV tu, nataka matokeo kwa Wananchi, tuko hapa hapa kuwatumikia wananchi hivyo nataka mkaanze kwa kasi pale wenzenu walipoachia," amesema Samia.