Rais Samia kuwagharimia matibabu watoto 100 

Muktasari:

  • Mgongo wazi na kichwa kikubwa ni tatizo linalowapata watoto, chanzo kikiwa ukosefu wa madini ya foliki asidi.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan atagharimia matibabu ya upasuaji na utengamao kwa watoto 100 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi yatakayofanyika katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amebainisha hayo leo Jumapili, Aprili 21, 2024 alipotembelea Taasisi ya MOI kuwajulia hali watoto 25 waliofanyiwa upasuaji chini ya ufadhili wa MO Dewji Foundation.

Amesema Rais Samia ameguswa na tatizo hilo na ameamua kugharimia matibabu ya watoto 100 zaidi, ili kuepusha madhara na ulemavu unaoweza kusababishwa na kuchelewa kufanyiwa upasuaji.

“Nimemsikia mwenyekiti wa chama cha wazazi na walezi wenye watoto wa tatizo hili la kichwa kikubwa na mgongo wazi, kwamba wana watoto kama 200 wanaopaswa kufanyiwa upasuaji lakini wazazi hawana uwezo.”

"Rais Samia amenielekeza nilete pesa kwa ajili ya watoto 100 ambao watafanyiwa upasuaji wa kichwa kikubwa na mgongo wazi bure kwa gharama zake," amesema Waziri Ummy katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya.

Amesema, "kwa hiyo Profesa Makubi wasilianeni na Chama cha wazazi na walezi wa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi Tanzania kujua watoto hawa ndani ya wiki moja, mbili wizara italeta hizo fedha za kugharimia matibabu au upasuaji na huduma za utengamao kwa watoto 100 kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.”

Ameipongeza MOI kwa kutoa matibabu ya watoto hao na MO Dewji Foundation kwa ufadhili wa matibabu ya watoto 50, akiwataka wadau kuendelea kujitokeza kusaidia wengine.

“Kubwa nataka kutoa wito kwa wazazi wenzangu, kwa wale wenye watoto wenye changamoto hii ya vichwa vikubwa na mgongo wazi wasiwafiche watoto hao, wahakikishe wanawapeleka kliniki ili wapate ushauri wa kitaalamu," amesema.

Daktari bingwa mbobezi wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu MOI, Dk Hamisi Shabani amesema tatizo la vichwa vikubwa linaweza kuzuilika kwa kuhakikisha wanaume wanawalisha wake zao vyakula vyenye madini ya foliki asidi na kuwawahisha kliniki kwa wale wenye tatizo hilo.

Mkurugenzi wa MO Dewji Foundation, Imran Sherali ameishukuru Serikali na taasisi ya MOI kwa kufanikisha matibabu hayo.

Amesema taasisi hiyo ipo tayari kuendelea kutoa msaada kwa watoto wengine.