Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia: Muswada bima ya afya kwa wote kupitishwa bungeni mwezi huu

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia katika Jubilee ya miaka 50 ya tangu kuanzishwa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (Wawata) katika Sherehe zilizofanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam leo Jumapili Septemba 11, 2022.

Muktasari:

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameweka wazi kuwa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote utapelekwa na kupitishwa bungeni mwezi huu.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameweka wazi kuwa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote utapelekwa na kupitishwa bungeni mwezi huu.

Bunge linatarajia kuanza vikao vyake Jumanne Septemba 13 mwaka huu jijini Dodoma.

Rais Samia amebainisha hayo leo Jumapili Septemba 11, 2022 wakati wa hafla ya kilele cha kusherekea za Miaka 50 ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (Wawata) zilizofanyika katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam huku akitoa wito kwa wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya.

“Nataka niwape habari njema kwamba Bunge litakalokaa mwezi huu wa tisa, linakwenda kupitisha muswada wa sheria ya bima ya afya kwa Watanzania wote…, kwa Watanzania wote” amesisitiza Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi amesema kuwa bima ya afya kwa wote itasaidia wananchi kupata matibabu kwa wakati.

“Niwaombe sana ndugu zangu, tutakapopitisha sheria hii, Watanzania twendeni tukajiunge na mifuko ya bima ya afya” amesema.

Pia, Rais Samaia amesema kuwa Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha mfuko utakaosimamia bima hiyo ufanye kazi kwa ufanisi na utasimamiwa na sheria na kanuni mpya.

“Nataka niwahakikishie, tunajua udhaifu wa mifuko yetu, tumechukua hatua tutakapoanza bima ya afya kwa wote mfuko utakaosimama kusimamia bima ya afya kwa wote utakuwa mfuko madhubuti wenye sheria na kanuni mpya ambazo zitafanya watu wote waweze kutibiwa katika viwango mbalimbali, mtu aweze kupata matibabu yote anayopaswa kupata” amebainisha

Kauli hiyo ya Rais Samia imekuja ikiwa ni siku 10 zimepita tangu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliposema kuwa wapo katika hatua za mwisho kukamilisha muswada wa bima ya afya kwa wote ambao unatarajiwa kupelekwa bungeni wakati wowote.

Septemba Mosi, 2022 katika mkutano wake na vyombo vya habari jijini Dodoma uliolenga kujibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa kuhusu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Waziri Ummy alitoa mwelekeo wa bima ya afya kwa wote akiahidi kuwa utapelekwa bungeni muda wowote.

“Tupo katika hatua za mwisho sana kuleta huu muswada na nitawaomba wananchi wawe tayari kujiunga na bima ya afya kwakuwa ugonjwa hausemi leo au kesho utaumwa unakuja bila taarifa.

“Tutakuja na kiwango kidogo cha kuchangia ambacho siwezi kusema sasa hivi, tutaweka kiwango tumefanya tathmini ya mfuko ifike mpaka miaka 10 au 30, tuingize watu wangapi, kwa mwaka watu wachangie kiasi gani na tutakuja na kiwango kidogo ambacho Watanzania wataweza kukimudu na hicho kiwango kitakuwa kinaonyesha wazi ni kiasi gani wanahitajika,” alisema Waziri Ummy.