RC Kagera aomba mkoa kuwa Kanda Maalumu ya Polisi

Kamishna wa Polisi Oparasheni na Mafunzo, Awadh Juma akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila wakishuhudia picha ya kituo cha polisi na nyumba ya mkuu wa kituo hicho vitakavyojengwa kata ya Bugarama.
Muktasari:
- Wastani wa mtu mmoja hufariki na kwa mwezi watu 28 hadi 30 hufariki dunia mkoani Kagera kutokana na matukio mbalimbali.
- Mkuu wa mkoa Kagera atoa maombi matatu kwa IGP amuomba Kamishna wa Polisi Operasheni na Mafunzo, Awadh Juma kuyafikisha maombi hayo ambayo ni Mkoa wa Kagera kuwa kanda maalumu, Bugarama kuwa Wilaya ya Kipolisi na ombi la askari zaidi ya 100.
Ngara. Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amemuomba Kamishna wa Polisi wa Oparasheni na Mafunzo nchini, Awadh Juma kufikisha ombi la Kagera kuwa kanda maalumu kutokana na mauaji yanayotokea kila siku wastani wa mtu mmoja na kwa mwezi watu 28 hadi 30.
Chalamila ametoa ombi hilo Mei 12, 2023 wakati Kampuni ya Tembo Nickel inayochimba madini ya Nickel Wilaya ya Ngara mkoani Kagera ilipokuwa ikisainiana mkataba wa makubaliano ya ulinzi na usalama kwa jamii na Jeshi la Polisi Tanzania mkataba uliofanyika Shule ya Msingi Bugarama wilayani Ngara.
Chalamila licha ya kuomba Kagera kuwa kanda maalumu pia ameomba kata ya Bugarama kuwa Wilaya ya Kipolisi kutokana na kata hiyo kujengwa kituo cha polisi chenye hadhi ya kituo cha mkoa na kuwa kutokana na kata hiyo kuwa mpakani yamekuwa yakijitokeza matukio mbalimbali ya uharifu.
“Niombe maombi machache kwako Kamishna wa Polisi utupelekee, najua kwa dhamana yangu ninao uwezo wa kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani lakini kabla sijazungumza naye na hii wewe uondoke nayo kwamba hapa kitajengwa kituo cha polisi chenye hadhi ya mkoa ambao atapaswa kukaa mtu mzito kidogo. Sasa niombe kwamba labda anzeni kuangalia mtu atakayekaa hapa naye aitwe mkuu wa polisi wilaya (OCD) maana yake oneni kama mnaweza kufanya wilaya maalumu ya kipolisi,” amesema.
Chalamila amekazia ombi lililotolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Wiliam Mwampagahle la kuongeza askari zaidi ya 100 katika kituo cha polisi kitakachojengwa Bugarama kutokana na kwamba askari hao watalinda maeneo ya mgodi masaa 24 pia watatakiwa kuwekwa maaskari katika mradi wa umeme Rusumo unaozihusisha nchi tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi na katika benki za CRDB na NMB zinazojengwa Rulenge.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Oparasheni na Mafunzo, Awadh Juma amesema kuwa, maombi aliyoyatoa mkuu wa mkoa kwa niamba ya Jeshi la Polisi ameyapokea na atayafikisha kwa kwa mkuu wa jeshi hilo nchini (IGP) na ombi la uanzishwaji wa wilaya ya kipolisi na uwepo wa askari wengi ni mambo yanayowezekana. Wanaweza kwenda nayo haraka ili kuhakikisha usalama wa eneo hilo unakuwepo na hasa wakizingatia kwamba wameishakuwa na uhakika wa kujengwa kituo kikubwa cha polisi chenye hadhi kubwa, usafiri na mambo mengine.
Kwa upande wake Meneja wa Mgodi wa Tembo Nickel, Manny Ramos ametaja mambo ambayo wamekubaliana kwenye mkataba kuwa ni pamoja na kuboresha kituo cha Polisi cha Bugarama kuwa daraja A, kuongeza kituo kidogo cha polisi katika Kijiji cha Muganza na nyumba za askari watakaokuwa wanafanya kazi katika jamii ya Tarafa ya Rulenge na kulipatia gari jeshi hilo katika kituo kitakachojengwa ambavyo thamani yake ni zaidi ya Sh1 bilioni na mkataba utakuwa wa miaka mitatu.