RC Kilimanjaro: Wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wazisalimishe
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka wananchi wa mkoa huo kusalimisha silaha wanazozimiliki kwa njia haramu katika vituo vya polisi au ofisi za Serikali.
Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka wananchi wa mkoa huo kusalimisha silaha wanazozimiliki kwa njia haramu katika vituo vya polisi au ofisi za Serikali.
Akizungumza na watendaji, wenyeviti wa vijiji pamoja na makatibu wa mashina wa CCM kwenye semina ya kuwajengea uwezo na kutambua majukumu yao ya kazi amesema adhabu ya kukutwa na silaha kinyume na sheria ni kifungo zaidi ya miaka 15.
"Kama unamiliki silaha ambayo sio yako tafadhali naomba mkazikabidhi silaha hizo kunako husika kabla sheria haijaanza kuchukua mkondo wake,"amesema RC Kagaigai
Naye kamanda wa polisi mkoani humo, Simoni Maigwa ametaka wananchi kutumia muda uliowekwa na Serikali katika kusalimisha silaha hizo kabla ya msako kufanyika.
Amesema Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, George Simbachawene ametoa muda wa mwenzi mmoja kuanzia Novemba mosi hadi 30 mwaka huu wananchi kusalimisha silaha kwa hiari na kwamba baadaye polisi itaendesha msako maalum na hatua za kisheria zitachukuliwa.
Soma zaidi:Siku 30 za Simbachawene kuhusu silaha