RC Kunenge ataka mahakimu wabanwe

Wafanyakazi wa Mahakama mbalimbali Mkoa wa Pwani wakiwa kwenye maandamano kuelekea viwanja vya Mahakama ya Mkoa huo kwa ajili ya maadhimisho ya kilele cha wiki ya sheria nchini. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • RC Pwani ataka Serikali kuwaondoa kazini mahakimu wanaoonyesha udhaifu katika kutoa hukumu.

Kibaha. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ametaka kuwepo utaratibu wa kuwabana mahakimu ambao rufaa zinazotokana na kesi walizohukumu awali zinatenguliwa kwenye mahakama za juu, ili kuongeza chachu ya uwajibikaji.

Kunenge ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari mosi, 2024 alipokuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya sheria iliyofanyika kibaha mkoani Pwani.

"Unakuta hakimu anahukumu kesi 100 na zinapokatiwa rufaa kwenye mahakama ya juu kesi 72 kati ya hizo hukumu zinabatilishwa, na hakimu huyo bado anabaki kuendelea na kazi hilo linapaswa kuangaliwa," amesema.

RC Pwani ataka Serikali kuwaondoa kazini mahakimu wanaoonyesha udhaifu katika kutoa hukumu.

Amesema kauli yake hiyo haina lengo la kuingilia utendaji wa mahakama bali matamanio yake ni kuona mahakimu waliopewa dhamana na Serikali wanatenda haki kwa kuzingatia ufanisi, na kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi.

Awali akizungumza katika maadhimisho hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Pwani, Joyce Mkhoi amesema juhudi za uharakishwaji wa kuendesha mashauri zimewezesha kupunguza msongamano wa mahabusu wanaopelekwa magereza ya Keko, Mkuza na Segerea kutoka 1,493 kwa mwaka 2022 na kufikia 740 mwaka 2023.

"Msongamano huu umewezekana kupungua kwa kiasi hiki kutokana na kujituma kwa maofisa hawa wa mahakama kwa kuhakikisha mashauri ambayo wana mamlaka nayo yanasikilizwa kwa wakati," amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) mkoa huo, Rita Nibwo ametaja baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kutetea watuhumiwa, kuwa ni pamoja na baadhi ya askari polisi kuwajumuisha kwenye tuhuma za wateja wao.

Naye Mkuu wa mashtaka mkoani hapa, Faraja Kiula amesema kuwa ili kufanikisha shughuli ya utoaji haki kwa wakati, kunahitaji ushirikiano wa wadau wakiwamo Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na waendesha mashitaka.

Wengine ni mashahidi, vielelezo Polisi, Magereza, Mahakama, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).