RC Malima: Rais Samia hajashindwa kujenga daraja la JPM
Muktasari:
- Ujenzi wa daraja la JPM linaloonganisha Wilaya za Misungwi na Sengerema mkoani Mwanza ulianza Februari, 2020 na kutarajiwa kukamilika Novemba 2024 badala ya Februari 2024 kwa sasa umefikia asilimia 63 likiwa na gharama ya zaidi ya Sh700 bilioni.
Mwanza. Serikali mkoani Mwanza imesema uvumi wa kusuasua kwa ujenzi wa daraja la JPM (Kigongo- Busisi) hazina ukweli huku ikionya wenye tabia ya kuiba vifaa vya kutengenezea daraja hilo.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza jana usiku Jumamosi Januari 14, 2023 eneo la Busisi wilayani Sengerema, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Adam Malima amesema Serikali haijashindwa kujenga na kukamilisha daraja hilo kama taarifa za baadhi ya watu wanaopotosha zinavyosema.
“Juzi nilipewa taarifa kuna malalamiko ya watu wa Kigongo-Busisi kwamba daraja haliendi na wanaona mradi umesimama, nikawaita wakandarasi hao wachina na baadaye nikamuita Meneja wa Tanroads mkoa wa Mwanza nikapata taarifa zao lakini na mimi nikapita kimya kimya kwenye daraja tukaja kuangalia maendeleo ya ujenzi,” alisema
“Watu walianza kuleta maneno, daraja litamshinda mama (Rais Samia) daraja halijamshinda mama, daraja lilichelewa kwa sababu ya vitu viwili, moja vifaa vinatoka china na kulikuwa na Uvuki-19 vikachelewa kidogo,” alisema
Alisema sababu nyingine ni udokozi wa vifaa vya kujengea daraja hilo unaoendelea akiwaonya wanaoiba vifaa hivyo kuacha mara moja kwakuwa wakikamatwa watachukuliwa hatua kali.
Alisema kuiba vifaa hivyo hawakomoi Serikalai, Rais Samia wala wachina bali wanajiibia wenyewe.
Awali, Meneja wa Wakala wa barabara nchini mkoani Mwanza, Ambrose Pascal alisema mpaka sasa ujenzi wa daraja huo umefikia asimia 63 akidai mkandarasi anafanya kazi usiku na mchana ili likamilike muda ulikokusudiwa.
“Kulikuwa na maneno yanaongelewa na wananchi wasio na nia njema wakisema Daraja letu la JPM linasua sua haliendi vizuri. Sisi tunafanya ukaguzi na Mkuu wa Mkoa alipita akafanya ukaguzi amejiomea daraja linaenda kwa kasi,” alisema
Ujenzi wa daraja la JPM linaloonganisha Wilaya za Misungwi na Sengerema mkoani Mwanza ulianza Februari, 2020 na kutarajiwa kukamilika Novemba 2024 badala ya Februari 2024 kutokana na ucheleweshwaji wa vifaa kutokana na janga la corona lililokuwa likikabiri dunia kwa gharama ya zaidi ya Sh700 bilioni.
Daraja hilo linalojengwa na Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) lina urefu wa kilomita 3.2 na litakapokamilika litapunguza muda wa kuvuka katika eneo hilo kutoka Saa moja inayotumika kwenye vivuko hadi dakika zisizozidi tano kwa njia ya gari.
Mkazi wa Busisi wilayani Sengerema, Kwandu Kija amesema taarifa za Serikali kushindwa mradi huo ziliwashtua kwakuwa licha ya kuwarahisishia safari lakini pia litachangamsha eneo lao na kuwa la kibiashara.