RC Mara awatimua kikaoni makatibu wa wabunge, asema…

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali, Suleiman Mzee akifungua kikao cha bodi ya barabara mkoa wa Mara leo Novemba 29, 2022 mjini Musoma.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee amewaondoka kwenye kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa huo makatibu wa wabunge ambao waliwawakilisha wabunge kwa maelezo kuwa makatibu hao siyo wajumbe halali wa kikao hicho huku akidai wabunge wengi wa mkoa huo wamekuwa na dharau na hawahudhurii vikao vya kisheria.

Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara (RC), Meja Jenerali Suleiman Mzee amewaondoa kwenye kikao cha bodi ya barabara wawakilishi sita wa wabunge wa Mkoa wa Mara kwa maelezo wabunge wa mkoa huo wamekuwa na tabia ya kutokuhudhuria vikao vingi mkoani humo.


Mkuu huyo wa mkoa amefanya maamuzi hayo leo Jumanne Novemba 29, 2022 muda mfupi kabla ya kuanza kwa kikao hicho ambacho kinafanyika ukumbi wa uwekezaji mjini Musoma na kusema makatibu wa wabunge sio wajumbe halali wa kikao hicho.


Amesema kwa muda mrefu wabunge wa Mkoa wa Mara wamekuwa na tabia ya kutokuhudhuria vikao ambavyo vipo kisheria jambo ambalo amedai ni dharau na kwamba halikubaliki.


"Haya ni mazoea mkoa huu una wabunge 10 wa majimbo pamoja na wale wa viti maalum, lakini wabunge mara zote hawahudhurii vikao hivi kwa hali hii hatuwezi kufika wanashindwa kuhudhuria vikao kwaajili ya maendeleo ya mkoa hii haikubaliki" amesema na kuongeza


"Mimi siwezi kumleta katibu wangu hapa aendeshe hiki kikao maana kama ni katibu hata mimi pia ninaye. Hakuna kitu kama hicho kila mtu kwa nafasi yake atimize wajibu wake na kwa yule mwenye udhuru atoe taarifa. Niwaombe wabunge waheshimu vikao hivi ambavyo vipo kisheria, kwanza vinawasaidia hata wao," amesema.


Akichangia kuhusu uamuzi huo, katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Lengael Akyoo amesema anaunga mkono uamuzi huo kwani wabunge wa mkoa huo ambao wengi wao wanatokana na chama hicho, wamekuwa na tabia ya kutokuhudhiria vikao vinavyofanyika mkoani humo.


"Sijawahi kusikia katibu wa mbunge amemuwakilisha mbunge bungeni lakini inapofika kwenye vikao tena vya kisheria, wakati wote wanawatuma makatibu wao hivi katibu anaweza kuwasilisha hoja za mbunge wake? Hii haikubaliki?" amesema.

Amesema umefika muda wabunge hao wanatakiwa kuheshimu sheria na kuhudhuria vikao ambavyo vinafanyika ndani ya mkoa huo kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya pamoja kwa ajili ya maendeleo ya mkoa wa Mara.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dk Vincent Mashinji ameunga mkono uamuzi huo na kusema historia inaonyesha wabunge hao wamekuwa na tabia ya kutokuhudburia vikao hivyo.


"Tangu nimkuja mkoa huu kila tukifanya vikao hivi wabunge hawahudhurii. Ifike mahala sasa sheria ifuatwe, kama wabunge hawapo, viti vyao vibaki wazi na endapo akidi haitatimia basi tujenge hoja ya kufanyika kwa marekebisho kuhusu wajumbe halali wa kikao hiki," amesema.

Dk Mashinji amesema siyo kweli kwamba wabunge wanakuwa hawapo jimboni au mkoani humo vinapofanyika vikao hivyo kwa maelezo wamekuwa wakiwaona wabunge hao kwenye wilaya zao ila wamefanya mazoea kutokuhudburia kwasababu yawezekana hawaoni umuhimu.

"Tunawaona mtaani wabunge wetu wengine hata jana tumewaona lakini unafika humu hawapo, makatibu wa wabunge sio wajumbe wa kikao hiki, wabunge wakumbushwe kutimiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kuhudhuria vikao hivyo ambavyo malengo yake pamoja na mambo mengine ni kujadili ilani ya uchaguzi ya CCM,” amesema

Mbunge wa Bunda, Mwita Getere ambaye ndiye pekee amehudhuria kikao hicho amesema badala ya wawakilishi hao kuondolewa kwenye kikao ni bora wakabaki kama waalikwa wa kawaida ombi ambalo mkuu wa mkoa amelikubali hata hivyo wawakilishi hao wameamua kuondoka ukumbuni.

"Lakini pia kikao hiki kiweke mambo sawa kwa mjumbe halali asipohudhuruia kikao anafanywaje, hebu tuweke mambo sawa DC au mkurugenzi wa halmashauri au mjumbe yeyote halali asipohudhuria kikao hiki," amesema.

Wawakilishi waliondolewa ukumbini ni pamoja na wa wabunge wa viti maalum, Juliana Masaburi, Agnes Marwa, Ghati Chomete pamoja na wale wa wabunge wa Bunda Mjini Robert Maboto, Musoma Mjini, Vedastus Mathayo, Tarime Mjini, Michael Kembaki.

Wabunge ambao hawajahudhuria kikao hicho wala kutuma wawakilishi ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum, Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, Mbunge wa Rorya, Jafari Chege, Mbunge wa Butiama, Jumanne Sagini na  Mbunge wa Mwibara, Charles Kajege.


Wengine ni Mbunge wa Serengeti, Amsabi Mrimi, Mbunge wa Musoma, Vijijini Profesa Sospeter Muhongo