RC Mndeme aitaka Kashwasa kutatua changamoto ya maji Kishapu

Muktasari:

  • Upatikanaji wa maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria unaowezeshwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Kahama- Shinyanga (Kashwasa) katika Jimbo la Kishapu lililopo mkoani Shinyanga umekuwa wa shida, ambapo hupatikana mara moja kwa wiki.

Shinyanga. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga (RC), Christina Mndeme amesema halidhishwi na utendaji wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Kahama Shinyanga (Kashwasa) katika shughuli za ugawaji maji, huku akiitaka kutatua changamoto ya kukata maji mara kwa mara Wilayani Kishapu.

Amesema hali hiyo inawafanya wananchi wakose maji na kushindwa  kuendelea kufanya shughuli za maendeleo na kujiongezea kipato.

Mndeme ameyasema hayo leo Jumamosi, Desemba 16, 2023 kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Shinyanga (RCC), kuwa Jimbo la Kishapu upatikanaji wa maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria yanayowezeshwa na Kashwasa ni wa shida.

Amedai kuwa kwa sasa huduma hiyo inapatikana mara moja kwa wiki.

"Serikali imetoa fedha zaidi ya Sh100 bilioni kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya maji Mkoa wa Shinyanga, niombe Kashwasa kufuta ratiba ya mgao wa maji, niwaombe kutatua haraka changamoto iliyopo," amesema Mndeme.

Mbunge wa Kishapu (CCM), Boniphace Butondo ameitaka mamlaka hiyo kutatua changamoto ya upatikanaji maji ili kujiepusha na ugonjwa wa kipindupindu na usumbufu kwa watumiaji.

Butondo ameeleza siku za hivi karibuni amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai kupata usumbufu, kushindwa  kuendesha shughuli mbalimbali za kibiashara zinazotegemea huduma ya maji.

“Hatupati maji inavyotakiwa, kwa wiki ni mara moja, wakati mwingine wiki mbili hatujapata maji ya Ziwa Victoria, ile maana ya kumtua mama ndoo kichwani tunaenda kuipoteza kabisa, hivyo tuwaombe Kashwasa muifanyie kazi Kishapu ili ipate maji ya kutosha.

"Serikali imetoa fedha nyingi za kuboresha huduma za maji hivyo niwaombe mfuatilie suala hili  kwa sababu kama ni fedha mmepata na mnafanya biashara, hivyo mnapaswa kuirudisha ije kuhudumia miradi ya wananchi,” amesisitiza Butondo.

Amesema mwaka wa fedha uliopita alifanya ziara akiwa na  Mkuu wa wilaya na mamlaka iliahidi mwaka huu wangetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa mabomba ya maji, ili kufanya ukarabati mkubwa jambo ambalo halijatekelezwa mpaka sasa.

Wakichangia hoja wajumbe wa kikao hicho akiwemo mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk Luzila John ameiomba Kashwasa kuwa na utaratibu wa kutoa ratiba ya uhakika ya upatikanaji maji,  ili kuwawezesha watumiaji kuhifadhi maji ya kutosha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Mhandisi Patrick Nzamba amekiri kuwepo kwa changamoto zilizosababisha mgao wa maji na kuahidi kuendelea kuzishughulikia ili kuondoa usumbufu unaojitokeza.

"Tatizo kubwa linalosababisha kukatika kwa maji mara kwa mara ni mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha maji kuwa na tope, lakini pia changamoto nyingine ni nguzo za umeme kuanguka na kusababisha kupungua kwa uzalishaji maji, ila tunaahidi kushughulikia kwa wakati ili wananchi wapate maji kila siku" amesema Nzamba.