Mbunge atakiwa kushughulikia kero ya maji kwanza

Muktasari:
- Wakizungumza na mbunge huyo wakati akikabidhi zawadi kwa washindi wakati wa fainali za mpira wa miguu kati ya Mageta FC na Seronga FC zilizofanyika mjini Mugumu wamesema wanalazimika kununua ndoo moja ya maji ya lita 20 kwa Sh500.
Serengeti. Wakazi wa jimbo la Serengeti mkoani Mara wamemuomba mbunge wao, Marwa Ryoba kushughulikia kero ya ukosefu wa maji inayowakabili kwa miezi minne.
Wakizungumza na mbunge huyo wakati akikabidhi zawadi kwa washindi wakati wa fainali za mpira wa miguu kati ya Mageta FC na Seronga FC zilizofanyika mjini Mugumu wamesema wanalazimika kununua ndoo moja ya maji ya lita 20 kwa Sh500.
Akijibu maombi hayo, Ryoba amesema taasisi husika zinaendelea kutatua kero ya maji.
“Nawaomba muwe wavumilivu wakati viongozi wenu tunashughulikia kero ya maji na mahitaji mengine muhimu ya kijamii,” alisema Ryoba.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Porini amesema uongozi umewasiliana na wataalamu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kutafuta ufumbuzi wa kuungua mara kwa mara kwa pampu ya kusukuma maji mjini Mugumu.
Meneja wa Mamlaka ya Maji Mugumu (Muguwasa), Mhandisi Dickson Gideon alisema wanafanya jitihada kuhakikisha usambazaji maji Mugumu unarejea katika hali ya kawaida.
Ametaja hitilafu ya umeme kuwa chanzo cha kuungua kwa pampu inayosambaza maji mjini humo.
Hata hivyo, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Tawi la Mugumu, Magoti Mtani alikana umeme unaosambazwa na shirika hilo kuwa chanzo cha kuungua kwa pampu za kusambaza maji mjini Mugumu na kuishauri Muguwasa na mzabuni aliyepewa kazi ya kufunga mtambo huo kufanya uchunguzi ili kubaini tatizo.