Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Mndeme: Maziwa ya kwanza hayana madhara nyonyesheni watoto

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme akiwagawia uji wa lishe watoto katika siku ya maadhimisho ya siku ya lishe na  unyonyeshaji Mkoa wa Shinyanga.

Muktasari:

Asilimia 30 tu ya akina mama mkoani Shinyanga wananyonyesha watoto wao ndani ya saa moja baada ya kujifungua, hivyo kusisitizwa kuwa maziwa ya mama kwa mtoto ni muhimu sana katika afya yake na ukuaji kimwili na kiakili.

Shinyanga. Wanawake mkoani Shinyanga wameshauriwa kunyonyesha watoto wao ndani ya saa moja wanapojifungua badala ya kukamua maziwa ya kwanza (yenye unjano) wakidhani yana madhara kwa mtoto.

Akizungumza Agosti 5, 2023 kwenye Maadhimisho ya siku ya Lishe na wiki ya unyonyeshaji yaliyofanyika Kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme amesema maziwa ya mama yana virutubisho pamoja na kinga ya mwili itakayoimarisha afya na kumuepusha mtoto na maradhi.

“Naomba mzingatie ushauri wa wataalamu wa afya kwamba mtoto akizaliwa baada ya saa moja anapaswa kunyonyeshwa na anyonyeshwe yale maziwa ya kwanza ya njano na siyo kuyakamua na kuyamwaga kwani yanavirutubisho hayana madhara yoyote kama wanavyodhani baadhi ya wazazi,

“Wanyonyesheni watoto ndani ya miezi sita bila kuwapa chakula chochote wala maji, isipokuwa labda akihitaji kunywa dawa usikilize ushauri wa daktari na wakati ukifika wa kumpatia vyakula vya ziada lizingatiwe suala la lishe bora ili akue kimwili na akili huku akiendelea kunyonyweshwa hadi afikishe miaka miwili,” amesema Mndeme

Mndeme amewataka pia waajiri wa sekta binafsi kutoa fursa kwa wafanyakazi ambao wamejifungua watoto kupata muda wa kunyonyesha ikiwa ni pamoja na kutengewa chumba maalumu kwa ajili ya kumhudumia mtoto akidai maziwa ya mama ni kinga bora, hupunguza tatizo la udumavu, utapiamlo na vifo vya watoto wachanga.

Akiongelea udumavu mkoani humo, Mndeme amesema tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano  limepungua, kutoka asilimia 32.1 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 27.5 mwaka 2022.

Ofisa Lishe Mkoa wa Shinyanga, Yusuph Hamisi amesema ni asilimia 30 tu ya akina mama mkoani humo wananyonyesha watoto wao ndani ya saa moja baada ya kujifungua, hivyo kuwasisitiza kuwa maziwa ya mama kwa mtoto ni muhimu sana katika afya yake na ukuaji kimwili na kiakili.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,  Johari Samizi amewataka wanawake kuendelea kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya katika suala zima la unyonyeshaji na lishe bora ili kuwakinga na maradhi.

Mmoja wa wanawake, Kareny Jamsoni ametoa ushuhuda kwa wanawake wenzake wa namna yeye na mume wake walivyozingatia suala ya unyonyeshaji kwa mtoto wake ndani ya miezi sita bila ya kumpatia kitu chochote kile cha kula na sasa ana Afya njema.