RC Shigela atua Geita, aomba ushirikiano

RC Shigela atua Geita, aomba ushirikiano

Muktasari:

  • Mkuu mpya wa mkoa mpya wa Geita, Martin Shigella amesema kipaumbele chake katika utumishi alioaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwatumikia wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili pamoja na kukusanya mapato.

Geita. Mkuu mpya wa mkoa mpya wa Geita, Martin Shigella amesema kipaumbele chake katika utumishi alioaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwatumikia wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili pamoja na kukusanya mapato.

Akizungumza mara baada ya kupokelewa mkoani humo na viongozi wa wilaya na watumishi wa sekretari ya mkoa, Shigella amewataka viongozi hao kuona ni wapi hawakufikia malengo ili waweze kuweka mikakati ya kufanya vizuri zaidi.

“Tutafsiri maono ya Rais yeye anataka kuona tunawatumikia wananchi, tunatatua changamoto zao, halmashauri tutafute mbinu za kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unaongezeka na tuboreshe shughuli za kiuchumi kwa wananchi,” alisema Shigella.

“Nimeambiwa hapa mnakata 122 ni wajibu wetu twende tuwafuate wananchi na sio tusubiri wao watufuate, fungueni milango tujadiliane tushirikishane kutatua changamoto za wananchi, msiogope kwenda kwa kiongozi kuwa mtaonekana wachonganishi hapana lengo letu ni kujenga na siwezi kujenga bila ushirikiano wenu,” alisema Shigela

Shigela amehamishiwa Geita kuchukua nafasi ya Rosemary Senyamule ambaye amehamishiwa Mkoa wa Dodoma.

Awali, kaimu katibu tawala mkoa huo, Herman Kapufi alisema mkoa huo wenye wakazi 1.7 milioni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 na hali ya makusanyo kutoka halmashauri sita za mkoa huo ni Sh 27.2bilioni sawa na asilimia 102.

Alisema mkoa huo unakabiliwa na upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali 7,600 kwani waliopo ni 15,147 kati ya 22,773 wanaohitajika.