Ridhiwani ashauri mazungumzo utatuzi wa migogoro kazini

Muktasari:
- Waziri Ridhiwani amesema si kila jambo linalotokea kwa mwajiriwa suluhisho liwe ni kumfukuza kazi au kumuundia tume kumjadili.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete ameshauri njia bora kwa waajiri kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi kwa waajiriwa wao, ni kutatua migogoro ya kazi kwa njia ya mazungumzo.
Ridhiwani amebainisha hayo leo Juni 19, 2025 wakati akifungua mkutano mkuu wa 66 wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wanachama pamoja na wadau wengine katika sekta hiyo.
Amesema si kila jambo linalotokea kwa mwajiriwa basi mwajiri aone suluhisho ni kumfukuza kazi au kumuundia tume kumjadili.
“Kama waajiri mkienda hivyo, mwishoni hamtafanikiwa,” amesema Ridhiwani huku akitoa rai kwa waajiri kufanya kazi yao vema, kwani hata migogoro inayotokea baina yao na waajiriwa haiwezi kufika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) au Mahakama ya Kazi.
Amesema waajiri wana nafasi ya kubaini changamoto za waajiriwa na kuzitafutia ufumbuzi na si kuwaza kumfukuza au kumuundia tume mwajiriwa kwa kuwa si kwenye kila jambo kunahitaji uamuzi huo.
“Mkishindwa kubaini changamoto za waajiriwa wenu, mtapata tabu,” amesema Kikwete akigusia pia mabadiliko ya sheria za kazi 2025 ambayo amesema yamezingatia kuongeza tija.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran alieleza namna mabadiliko ya sheria za kazi yalivyowavutia waajiri.
Amesema mwaka 2024, waajiri walifahamishwa juu ya marekebisho ya sheria za kazi za Tanzania ikiwa ni pamoja na Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini (Sura ya 366), Sheria ya Taasisi za Kazi (Sura ya 300) na Wasiokuwa raia (Kanuni ya Ajira) Sura. 436} yenye lengo la kukuza mazingira ya haki na jumuishi zaidi.
“Mwaka huu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi 2024, unaojumuisha kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa wanawake wanaojifungua watoto njiti kutoka wiki 36 hadi 40.
“Vilevile kutoa likizo ya siku saba kwa akina baba wa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati,” amesema na kuongeza kuwa ATE inajivunia kuwa sehemu ya mchakato wa utetezi uliosababisha marekebisho hayo.
“Si haya pekee, maeneo mengi yameboreshwa katika nyanja tofauti ikiwamo kwa wahitimu wanaotafuta uzoefu wa kazi, wafanyakazi katika miradi ya muda, wafanyakazi wa msimu, wasio raia wenye vibali vichache vya kazi na kuruhusu uwazi wa kisheria na ulinzi kwa wafanyakazi katika majukumu yasiyo ya kudumu.
Amesema zaidi ya hayo, waajiri hawawezi kuanzisha au kuendeleza mashauri ya kinidhamu dhidi ya mwajiriwa ikiwa mgogoro tayari uko mbele ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) au Mahakama ya Kazi.
Pia, amesema mabadiliko hayo yanatoa fursa kwa waajiri na waajiriwa kujadili masharti maalumu wakati wa milipuko ya magonjwa ya kuambukiza au dharura nyinginezo.
“Kama ilivyotokea wakati wa Uviko-19, sasa mnaweza kujadiliana na ajira ya mfanyakazi ikabaki salama baada ya majanga,” amesema.