Ridhiwani Kikwete ataja sababu kuomba msaada ughaibuni

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mboga, Ester Elanga akionyesha umahiri wa kutumia kompyuta mpakato kwa mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:


  • Naibu Waziri, Ridhiwani Kikwete amepokea msaada wa kompyuta 80 na vifaa vya umeme jua kwa shule za sekondari Bagamoyo, ambavyo vitasaidia kuboresha elimu na kukabiliana na changamoto za teknolojia na umeme shuleni.

Bagamoyo. Ongezeko la mahitaji ya vifaa vya   Tehama kama nyenzo  ya kufundishia wanafunzi  kwenye shule za sekondari nchini, ni moja ya sababu zilizomlazimu Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete kuomba msaada wa kompyuta mpakato ughaibuni.

 Kikwete ambaye pia ni mbunge wa Chalinze mkoani Pwani, ameeleza changamoto nyingine ambayo ilikuwa ikimnyima usingizi ni ukosefu wa umeme kwenye Shule ya Sekondari  Jakaya Kikwete iliyopo wilayani  Bagamoyo ambayo sasa imepatiwa ufumbuzi  baada ya kupata wadau waliotoa  vifaa vya umeme jua na kufunga kwenye shule hiyo.

Ametoa kauli hiyo  leo, Februari 23,2024 wakati akipokea msaada wa mradi  wa vifaa vya umeme jua na kompyuta kutoka taasisi mbili za Reneal International education outreach na Matheostechs kwa ajili ya kusaidia sekondari wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

"Dunia ya sasa inatulazimu kujikita kwenye matumizi   Tehama karibu maeneo yote, kwa kutambua hilo nililazimika kuwatafuta hawa ndugu zetu na kuwaomba msaada wa kompyuta mpakato na leo wametupatia kompyuta 80, ili zitumike kuwafundishia wanafunzi wetu sekondari," amesema.

Akiwa Shule ya Sekondari Jakaya Kikwete, mbunge huyo ameishukuru taasisi ya Metheostechs iliyofanikisha kuondoa changamoto ya ukosefu wa umeme, baada ya kutoa vifaa na kufunga mfumo mzima na sasa huduma hiyo imetengamaa.

"Jina la shule hii ni kubwa, ilikuwa aibu kukosa huduma ya umeme, hivyo hawa ndugu zetu wametusaidia katika hilo na sasa wanafunzi wataweza kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi,” amesema.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa shirika lisilo la Serikali Reneal International kutoka nchini Marekani, David Nyangaka amesema msaada wa kompyuta mpakato 80 zilizotolewa na taasisi hiyo zimegharimu Sh71 milioni na zinagawiwa kwa sekondari nne ambazo ni Mboga, Msata, Mdaula na Mandela.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa taasisi ya Matheostechs, Matheo Malya anasema wamesaidia shule hiyo kuwa na huduma ya umeme ili kuunga mkono juhudi za Serikali kupunguza changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini.

Amesema taasisi hiyo imetoa msaada wa mitambo na kufunga mfumo mzima ambao gharama yake ni Sh16.8 milioni na anaamini hali hiyo itawarahisishia wanafunzi kujifunza na kuinua kiwango cha ufaulu hasa masomo ya sayansi.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mboga, Tobati Lutengwe amesema vifaa hivyo vitawarahisishia kujifunza, kwani ukilinganisha na awali masomo yote walikuwa wakitumia makaratasi.