Ripoti maalumu: Kibarua kigumu cha hesabu za mapato, marejesho ya mkopo mwendokasi - 2

Baadhi ya mabasi ya mwendoharaka yakifanya safari zake jijini Dar es Salaam. Picha na maktaba.

Muktasari:

  • Baadhi ya wamiliki wa daladala Dar es Salaam wataka kuwa sehemu ya kumiliki hisa kama fursa hiyo itatolewa tena.

Dar es Salaam. Baada ya ripoti maalumu ya huduma za usafiri wa mwendo haraka jana kubainisha mazingira magumu ya huduma hizo kwa abiria, leo tutaangazia eneo la hesabu za mapato na gharama za uendeshaji wa mradi huo. 

Kwa mujibu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), miongoni mwa mafanikio mengine ni ongezeko la mapato ya nauli zinazoingia kwenye mfumo. 

Katika ufafanuzi wake, Ofisa Uhusiano wa Dart, William Gatambi aliliambia gazeti hili tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa kielektroniki wa kukusanya nauli (AFCS) kumekuwepo na ongezeko la mapato yatokanayo na nauli. 

Bila kuhusisha idadi ya mabasi yaliyotumika Julai 2021 hadi Juni 2022, alisema Dart imekusanya Sh36.2bilioni, sawa na makadirio ya Sh3bilioni kwa mwezi. Endapo wakala huo utakuwa umekusanya kwa makadirio hayo ya kila mwezi, wastani wa Sh253bilioni ndani ya miaka saba ya huduma hiyo. 

Mwenendo huo wa makusanyo unajitokeza wakati Serikali ikitakiwa kurejesha mkopo wa Benki ya Dunia (WB) wa dola 235 milioni (Sh580bilioni) za ujenzi awamu ya kwanza iliyoanza huduma Mei, 2016. 

Baadhi ya wadau walisema mafanikio ya mapato hayo yanatakiwa kupimwa katika uhusiano wa gharama za uendeshaji wa mradi ikiwamo uhai wa mabasi na athari zake.

“Uhai wa mabasi hayo ni miaka mitano tu, haitakiwi kuzidi muda huo, yakizidisha umri huo matokeo ni kutumia bajeti kubwa kwa ajili ya matengenezo kuliko mapato inayoingiza,” alisema Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Profesa Zacharia Mganilwa alipohojiwa kuhusu uhai wa mabasi hayo. 

“Kwa miaka mitano ya awali, gharama zitakuwa kawaida, lakini baada ya miaka hiyo mitano zitaanza kupanda. Kwa mfano kama basi moja linalozalisha Sh400milioni lakini matengenezo litahitaji Sh800milioni, ndio msingi wa mabasi mengi kupaki kwa sasa. Hakuna sababu nyingine ya kupaki.” 

Profesa Mganilwa anatoa angalizo hilo wakati mvua zinazoendelea kunyesha katika jiji hilo zikiendelea kutengeneza hasara kwa wakala huo hatua inayoathiri ufanisi na mwenendo wa mapato. 

Kwa mfano, mvua zilizonyesha Aprili, 2017 katika jiji hilo ziliharibu miundombinu na magari ya Udart huku Sh400 milioni zikitumika kwenye matengenezo ya mabasi kama ilivyonukuliwa na gazeti hili. Hii inamaanisha kwa miaka saba, huenda wakala huo umetumia wastani wa Sh2bilioni.  

Profesa Mganilwa anatoa angalizo katika mradi huo. “Tatizo lililopo naliona maeneo mengi, haiwezekani mhasibu kuongoza ofisi ya sheria au mwanasheria kuongoza ofisi ya CAG.” 

Sakata la ubia 

Kuhusu ubia, wadau wanasema msingi wa changamoto hizo zinazoendelea kwa abiria unachochewa na dosari za ubia licha ya wakala huo kujivunia mafanikio mbalimbali iliyoyapata kwa uwekezaji huo. 

Awali Serikali ilionyesha dhamira ya kuwezesha wazawa katika mradi huo lakini wamiliki hao wa daladala wameibua hoja ya usaliti na kukosekana utayari ndio chanzo cha mkwamo wa kufanikisha ubia huo.    

Kabla ya kuanza mradi huo, mwaka 2014 wamiliki wa daladala waliingia ubia kati yao na Kampuni ya Simon Group iliyonunua asilimia 51 ya hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda). 

Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Mabrouk Sabri anasema mkataba huo uliwataka wamiliki wa daladala kumiliki asilimia 30 ya hisa za Kampuni ya UDART(ambazo ni asilimia 51) ili kunufaika na zabuni ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (Dart) lakini hazikutosha.  

“Tulitakiwa kununua asilimia 30 ya hisa za kampuni ndani ya miaka mitatu lakini tulikwama, ilikuwa ni jambo geni na haikuwa lazima, kwa hiyo hutukuweza kulazimisha watu wanunue hisa. Serikali ilitoa nafasi lakini tulishindwa wenyewe. Kama Serikali itatoa nafasi nyingine ni jambo jema,”alisema Sabri. 

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Uwadar), Kismat Vatfad alitofautiana na hoja hiyo akisema baadhi yao walisaliti na kuanza kutumikia mwekezaji. 

“Huo mradi unaoendelea ulitakiwa kuwa chini ya wamiliki wa daladala lakini tukavurugana wenyewe, baada ya kusaini mkataba na kampuni ya Simon, wanachama walinunua sehemu ya asilimia 51 ya hisa hizo kwa zaidi ya Sh2bilioni lakini hadi sasa haijulikani zilipo, kuna usaliti ulitokea,”alisema Vatfad. 

“Viongozi wa Chama cha Wamiliki wa Daladala (Uwadar) na Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa) walitakiwa kuwa sehemu ya wajumbe kwenye bodi ya kampuni hiyo badala yake kampuni ikaamua kumuajiri mmoja kati ya wawakilishi hao. Mradi ukaanza kuyumba.” 

Pili, Vatfad alisema changanmoto nyingine ilikuwa ni mazingira ya harufu za rushwa katika mchakato wa upatikanaji mkopo wa mwekezaji, hesabu za uendeshaji kabla ya kuanza kuyumba uendeshaji. 

Hata hivyo Mei 2018, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliliambia Bunge kuhusu mpango wa kukishirikisha Chama cha Wamiliki wa Daladala (Uwadar) kuwa miongoni mwa watoa huduma katika mradi huo ili kupunguza kero za usafiri huku akiahidi kumwondoa mwendeshaji wa sasa iwapo itabainika ana tatizo. 

Februari 13, mwaka huo, Udart ilitangaza kupokea mabasi ya mwendokasi 70 yenye thamani ya Dola za Marekani 270,000 kutoka China lakini Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania (TRA) iliyashirikilia mabasi hayo kwa zaidi ya mwaka mmoja katika Bandari ya Dar es Salaam baada ya kushindwa kulipiwa ushuru. 

Pamoja na changamoto hizo, Simon Group ilipinga mwekezaji mwenza mahakamani lakini Serikali ilishinda kesi hiyo. Vyanzo vinaeleza kwa sasa Serikali inamiliki asilimia 85 ya hisa za Udart huku Kampuni ya Simon ikibakia na asilimia 15 hatua inayoathiri mfumo wa mauzo ya hisa soko la DSE. 

“Lakini ukweli ni kwamba Serikali haitakiwi ifanye biashara, ila iweke mazingira mazuri ya biashara kwa ajili ya sekta binafsi, endapo Serikali itaendelea kuendesha mradi huo, hautalipa na jamii haitanufaika na huduma kama inavyokusudiwa,”alisema Profesa Mganilwa alipogusia eneo hilo kiuzoefu. 

Hofu na matumaini 

Kutokana na mkwamo huo, baadhi yao wameachana na biashara ya daladala na kuhamia kwenye mabasi ya mikoani baada ya kukosa fursa katika awamu ya kwanza ya mradi huo.

“Mimi nilikuwa na daladalaa 40, nimeuza nimebakiza 10 tu, nimehamia kwenye biashara ya mabasi makubwa,”alisema Vatfad. 

Hali hiyo inajitokeza wakati Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabarani wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Johansen Kahatano akisema daladala 2,461 kati ya 10,100 zitaondolewa katika barabara ya Kilwa ili kupisha mradi wa awamu ya pili itakayohudumia angalau abiria 600,000 kwa siku.    

Kuhusu mradi huo kuanza: “Bado Serikali haijatangaza zabuni kwa ajili ya manunuzi ya mabasi hayo, lakini kwa sasa iko kwenye maandalizi,” alisema Ofisa Uhusiano wa Dart, William Gatambi alipoulizwa kuhusu hatua hizo. 

Gatambi alisema uendeshaji na utoaji huduma za mradi huo unachochea ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP). 

“Aidha, mfumo wa Dart unatoa fursa na kuvutia wafadhili, wadau kuwekeza kwenye miundombinu, huduma za usafiri na kuendesha shughuli za kiuchumi katika mfumo, ushiriki wa sekta binafsi umevutia uwekezaji na msongamano wa magari umepungua hususani barabara ya Morogoro,”anasema. 

Akifafanua, Kamishna wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila alisema Serikali inatamani kuona wazawa wakiwa sehemu ya uwekezaji huo.

“Wamiliki hao wakiingia kwenye ubia ni sehemu ya kuchachua uchumi wa Taifa, utaratibu wa kisheria uliopo ni kwamba, wanaweza kuandika andiko la mradi ili kushawishi namna gani wanaweza kushiriki.” 

“Timu ya watalaamu itachambua na majadiliano yataanza kwa pande mbili. Wanaweza kujitokeza kwa utaratibu wa kikundi wakiwa na kampuni au mtu binafsi pia, Serikali iko wazi. Lakini hatutazami suala la mitaji ila andiko lao la upembuzi yakinifu, ndio tafsiri ya PPP. Hii ni fursa kwao wajenge ushwishi tu.” 

Mmiliki wa daladala, Break Salim Break alisema bado anaamini uwezekano wa ubia katika mradi huo. Aliomba Serikali itoe majaribio ya njia kadhaa ili kuthibitsha ufanisi wa huduma katika mradi huo. 

“Humu kwenye biashra ya daladala wapo watu wanamiliki hadi daldala 70, sembuse hizo gari, watupe hata njia moja waone kama hatutaweza, tunachohitaji ni dhamana tu ya serikali ili tuweze kukopesheka benki, kwani hata hizi daladala hakuna anyenunua kutoka hela za mfukoni,”alisema Break.