Rugambwa ateuliwa kuwa Askofu Mkuu mrithi wa Jimbo Kuu la Tabora
Askofu Mkuu Protase Rugambwa
Muktasari:
- Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amemteua Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu Mkuu mrithi (coadjutor) wa Jimbo Kuu la Tabora.
Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amemteua Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu Mkuu mrithi (coadjutor) wa Jimbo kuu la Tabora.
Taarifa ya uteuzi huo imetolewa leo Aprili 13, 2023 na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima.
Kabla ya uteuzi huo Askofu Rugambwa aliwahi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma tangu mwaka 2008 hadi mwaka 2012 pamoja na Katibu Mkuu wa Congregasio ya Uinjilishaji Vatican.
Kwa mujibu wa tovuti ya Vatican Radio, Askofu Rugambwa alizaliwa Mei 31, 1960 mkoani Kagera na alipata daraja la upadri kutoka katika Seminari ndogo za Katoke iliyoko Rulenge-Ngara na Itaga.
Pia alisoma masomo ya falsafa katika Seminari Kuu ya Kibosho iliyoko Jimbo Katoliki la Moshi na baada ya kuhitimu masomo yake Septemba 2, 1990 alipadrishwa kisha alifanya utume parokiani, Seminari Ndogo ya Katoke, Mwenyekiti wa Idara la Liturjia Jimbo Katoliki Rulenge na Mhudumu wa shughuli za kiroho Hospitali ya Biharamulo.
Kuanzia mwaka 1994 hadi 1999 alipelekwa mjini Roma kwa masomo kwa masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano na kujipatia Shahada ya Uzalimivu katika shughuli za kichungaji.