Runinga kutumika mapambano ya kipindupindu

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  Dk Thomas Rutachunzibwa (kulia) akipokea runinga iliyotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya. Jumla ya runinga 57 zimetolewa kwenye mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu, Kagera, na Singida. Picha na Saada Amir

Muktasari:

  • Wizara ya Afya na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wameanzisha kampeni ya elimu kwa umma kuhusu magonjwa ya milipuko kwa kutoa runinga 57 kwenye vituo vya afya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mwanza. Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wamezindua kampeni ya elimu kwa umma kwa kutoa runinga 57 kwenye vituo vya afya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa nchini Tanzania.

Hatua hii inalenga kuwawezesha wananchi kujifunza jinsi ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hasa wakati wa mlipuko wa kipindupindu katika mikoa ya Mwanza, Simiyu, Kagera, Geita, na Shinyanga.

Runinga hizo zitasaidia kutoa elimu kwa wananchi wakati wanaposubiri matibabu na kuelimisha kuhusu masuala ya afya na hatua za kujikinga na magonjwa.

Mradi wa REA pia unasambaza umeme katika vituo vya afya na pampu za maji vijijini kwa lengo la kuboresha huduma za afya na maji katika maeneo ya vijijini.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa amesema leo Jumatano Februari 7, 2024 wakati wa makabidhiano ya runinga hizo, kuwa vifaa hivyo vitasaidia kufikisha ujumbe kuhusu masuala ya afya, hasa kipindi hiki tunachopambana na milipuko ya magonjwa kama kipindupindu na ugonjwa wa macho (red eyes)

Ofisa Uhusiano wa REA, Jaina Msuya amesema “mradi huu wenye thamani ya Sh37.4 bilioni unafikia jumla ya vituo vya afya 57 na unahusisha pampu za maji 363 ambazo zimesambaa mikoa mbalimbali.