Rushwa yatajwa kulea uhalifu wa dawa za kulevya
Muktasari:
- DCEA, Takukuru zameunganisha nguvu kupambana na rushwa na biashara ya dawa za kulevya baada ya kubainika aina hiyo ya uhalifu una uhusiano mkubwa.
Dar es Salaam. Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema kuna uhusiano mkubwa kati ya rushwa na biashara ya dawa za kulevya kwa kuwa wafanyabiashara wa dawa hizo haramu hutumia rushwa kufanikisha uhalifu huo.
Kutokana na hilo amesema kuna umuhimu mkubwa wa DCEA na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kushirikiana katika utoaji elimu madhubuti inayopinga rushwa na dawa za kulevya.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema hayo leo Jumamosi, Februari 24, 2024 jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo kwa maofisa waelimishaji wa Takukuru katika mkoa na wilaya zote nchini, yaliyofanyika kwa lengo la kujengeana uwezo na kupeana mbinu zaidi za uelimishaji umma katika mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya.
Amesema tatizo la dawa za kulevya na vitendo vya rushwa, ni tatizo mtambuka linalohitaji ushiriki wa pamoja kukabiliana nalo kwa kuwa ni uhalifu unaohusisha mtandao wa wafanyabiashara wakubwa.
Kamishna Jenerali Lyimo ametoa wito kwa wadau wote kutambua kwamba elimu ni moja nyenzo muhimu ya kukabiliana na changamoto hizo, hivyo maofisa wa DCEA, maofisa wa Takukuru, wakuu wa shule na vyuo, walimu, walezi wa vilabu, vyombo vya habari, wasanii, vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi wote washirikiane kupinga rushwa na dawa za kulevya.
“Tumeshuhudia maofisa wa Takukuru na Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wakishirikiana kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya kijamii nchini, hali ambayo itasaidia kuongeza uelewa juu ya athari za ya rushwa na matumizi na biashara ya dawa za kulevya” amesema Lyimo.
Akizungumzia mafunzo hayo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Neema Makalyelye amesema matunda ya mafunzo hayo yataonekana katika utendaji kazi wa waelimishaji watakaporejea katika vituo vyao vya kazi.
Amesema washiriki wamepitishwa katika andiko maalumu la kampeni ya kutokomeza rushwa na dawa za kulevya katika shule na vyuo nchini pamoja na kuelimishwa uhusiano uliopo kati ya dawa za kulevya na rushwa, ili waweze kutumia nyenzo hizo katika vituo vyao kufanya kazi.
“Katika siku tatu za mafunzo, washiriki walijifunza kuhusu tatizo la dawa za kulevya, makundi ya dawa za kulevya, sababu za matumizi, namna ya kumtambua mtumiaji wa dawa za kulevya, kuzitambua dawa tiba zenye asili ya kulevya, uraibu wa dawa za kulevya, magonjwa ambukizi na tiba saidizi kwa kutumia dawa. Pia wamejifunza namna ya kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na uwepo wa huduma katika nyumba za upataji nafuu,” amesema Neema.
Ushirikiano wa DCEA na Takukuru ni utekelezaji wa agizo la Serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzitaka taasisi hizo kuunganisha nguvu kutoa elimu juu ya athari za vitendo vya rushwa na biashara ya dawa za kulevya kwa kuweka mkazo kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuoni kupitia klabu za kupinga rushwa.