Ruto ashinda kituo walichopiga kura familia ya Kenyatta

Muktasari:

  • Licha ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kuwataka Wakenya wasimpe kura mgombea urais wa Kenya Kwanza na Naibu Rais, William Ruto bali wampe kura hizo mgombea urais wa Azimio la Umoja, Raila Odinga ameshindwa kumbeba mgombea huyo katika kituo alichopigia kura

Nairobi. Licha ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kuwataka Wakenya wasimpe kura mgombea urais wa Kenya Kwanza na Naibu Rais, William Ruto bali wampe kura hizo mgombea urais wa Azimio la Umoja, Raila Odinga ameshindwa kumbeba mgombea huyo katika kituo alichopigia kura

Matokeo ya kura za urais ya uchaguzi mkuu, uliofanyika jana nchini humo, yanaonyesha katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya msingi Mutomo katika jimbo la Gatundu Kusini ambako Rais Kenyatta na familia yake (mama yake Ngina Kenyatta na mkewe Margareth Kenyatta) walipigia kura yanaonyesha Ruto amepata kura mara mbili zaidi ya alizopata Odinga huku kura tatu zikiharibika.

Matokeo hayo pia yameonyesha kuwa mgombea wa urais wa chama cha Agano, Waihiga Mwaure amepata kura nne huku mgombea urais wa chama cha Roots, George Wajackoya amepata kura tisa.

Katika kura zilizopigwa na kuhesabiwa kituoni hapo zinaonyesha kuwa Ruto amepata kura 983 huku Odinga amepata kura 464

Waliojiandikisha kupiga kura katika kituo hicho walikuwa ni wapigakura 2,164 lakini waliojitokeza ni 1,460.