Saa 48 za uamuzi, vigogo Chadema wakijifungia

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inatarajiwa kujifungia kwa siku mbili kuanzia leo kuandaa Azimio la Mtwara la kushiriki au kutokushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu.
Pia, kikao hicho kitakachohitimishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kitafanya tathimini ya maandamano ya amani waliyoyafanya katika majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha.
Februari 27 mwaka huu, Mbowe akihutubia mamia ya wananchi viwanja vya Reli, Arusha katika maandamano ya amani alisema wanakwenda kujifungia mkoani Mtwara kufanya tathimini ya maandamano hayo na mikakati mingine ya chama.
Lengo la maandamano hayo yaliyopewa jina la ‘Vuguvugu la haki ya Watanzania’ ni kuishinikiza Serikali kushughulikia gharama za maisha kwa madai kuwa, yamekuwa magumu kutokana na mfumo wa bei za bidhaa mbalimbali.
Mbali na hilo, walikuwa wakipinga miswada ya uchaguzi iliyokuwa imepelekwa bungeni Novemba 10 mwaka jana wakitaka iondolewe wakidai haikushirikisha wadau mbalimbali.
Hata hivyo, katika mkutano wa Bunge uliopita, miswada hiyo ilijadiliwa kisha ikapitishwa na inasubiri kusainiwa na Rais.
Miswada hiyo ni muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023.
Jana, mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu akizungumza na gazeti hili lililotaka kujua kinachoendelea alisema, “tayari vikao vya sekretarieti vimemalizika na kamati kuu itakutana kwa siku mbili kuanzia kesho (leo) yaani Machi 5 na 6.”
“Wajumbe wa kamati kuu tunaanza kuingia leo (jana), tunakwenda kujifungia kwa siku mbili, tutatoka na Azimio la Mtwara ambalo litatolewa Mtwara kama alivyosema mwenyekiti kuwa litakuwa Azimio la Mtwara,” alisema.
Mjumbe huyo wa kamati kuu ambaye hakutaka kuandikwa jina lake, alisema pamoja na mambo mengine, “tutaangazia maendeleo ya Chadema Digital imefikia wapi, tutajadili ushiriki wetu au kutoshirikia kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na tutaangalia uchaguzi wetu wa ndani unaoendelea.”
Alipoulizwa uchaguzi huo wa ndani umefikia hatua gani, alijibu, “kwa sasa umefikia ngazi ya wilaya na kanda moja ya Magharibi yenyewe imefikia ngazi ya mkoa na kinachosubiriwa ni kutangazwa kwa tarehe ya uchaguzi wa kanda. Nafikiri uchaguzi ngazi ya Taifa utakuwa Juni au Julai mwaka huu.”
Kuhusu maandamano, alisema, “Azimio la Mtwara litatutabanaisha kwa wananchi tunakwendaje kwa sasa, kama ni maandamano yatakuwa ya mfumo upi ni huuhuu ama tubadili.”
Gazeti hili, lilimtafuta Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu kujua sababu za kufanya mkutano Mtwara alisema, “hatujawahi kuwa na vikao vya siri muda ukianza na ukiisha tutaueleza umma. Naomba sana kuweni na subra tutasema."
Alipoulizwa jana Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, Benson Kigaila alijibu,” saa hizi siwezi (jioni) kukueleza chochote kwa sababu nipo kwenye kikao hapa Mtwara, nikimaliza naweza kuwa na wakati mzuri wa kukueleza kuhusu na maswali unayoniuliza."