Mpambano Pambalu, Wenje Nyamagana

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana Februari 15, 2024 katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  • Ezekia Wenje ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria aliwahi kuwa mbunge wa Nyamagana, huku John Pambalu akiwa diwani wa Butimba, jijini Mwanza kati ya mwaka 2015 hadi 2020.

Mwanza. Hapatoshi ubunge Nyamagana kati ya Ezekia Wenje na John Pambalu mwaka 2025, ndivyo unavyoweza kueleza kutokana na makada hao wa Chadema kuonyesha nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu 2025.

 Wakati Pambalu, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa la Chadema (Bavicha) akitangaza jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza kugombea ubunge kwenye jimbo hilo, Wenje ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria anatajwa kuonyesha nia hiyo, ingawa mwenyewe anasema muda ukifika atatangaza ni wapi atagombea.

Akizungumza jana, Februari 15, 2024 katika mkutano huo, Pambalu amesema atasimama tena Nyamagana kuwania nafasi hiyo, huku akiwataka wananchi kupigania Katiba mpya na mabadiliko ya sheria za uchaguzi.

“Mwenyekiti (Freeman Mbowe) niligombea ubunge Nyamagana na kilichotokea kinajulikana… tupiganie Katiba mpya, tupiganie sheria mpya zibadilike na nitasimama tena Nyamagana,” amesema Pambalu.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa la Chadema (Bavicha), John Pambalu akizungumza jana, Februari 15, 2024 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza. Picha na Anania Kajuni

Maelezo hayo ameyasisitiza pia leo Ijumaa, Februari 16, 2024 kwenye mahojiano na Mwananchi, huku akisisitiza wengine wanaotamani nafasi hiyo kujitokeza kwa kuwa ni jambo la kidemokrasia.

“Mimi ni mwanasiasa na mzaliwa wa Nyamagana na nimepata fursa ya kuongoza Nyamagana, pia nikiwa diwani, kwa hiyo ninatamani kugombea tena hapa kwa sababu kwanza ni nyumbani, pili kuna maono ambayo nilikuwa nahitaji kuyaona yakitekelezeka,” amesema Pambalu.

Pambalu aliyewahi kuwa diwani wa Butimba, jijini Mwanza mwaka 2015 na kugombea ubunge mwaka 2020 amesema akipata fursa ya kurudi na kuchaguliwa na wananchi kuwa mbunge wa jimbo hilo watarajie kupata mbunge msemaji wa kero za watu.

Amezitaja kero hizo kuwa ni pamoja na miundombinu ya barabara, maji na miundombinu mibovu katika maeneo waliyopelekwa wafanyabiashara wadogo (machinga) kufanyia shuguli zao.

“Pili vipaumbele vyangu vya mwaka 2020 havijafanyiwa kazi hata kidogo, ubovu wa miundombinu ya Nyamagana kwa mfano; barabara inayotoka Igoma-Buhongwa-Kishiri na Lwahnima, barabara kutoka Bugando mpaka Mahna Kati, barabara inayotoka Butimba, Mahina mpaka Mandu,” amesema.

Kuhusu wengine kutajwa kuwania nafasi hiyo Nyamagana akiwemo Wenje aliyewahi kuwa mbunge wa Nyamagana (2010 – 2015), kisha 2020 kugombea Rorya mkoani Mara, Pambalu amesema, “Hiki kinaitwa Chama cha Demokrasia na demokrasia ni ushindani, pia mimi nina imani na nina hakika natosha.”  

Akizungumzia madai ya kuwa miongoni mwa wanaotaka kugombea ubunge Nyamagana, Wenje amesema atagombea, lakini kuhusu atagombea wapi atazungumza wakati wa kutangaza nia ukifika.

“Kwanza kuna process (taratibu) ya kuwapata wagombea kwenye vyama vyetu ambayo ni kura ya maoni, kwa hiyo hata nikisema nitagombea Ukerewe bado nitapitia kwenye kura ya maoni.

“Kwa hiyo unaweza kufikiria kwenda kugombea sehemu fulani ukashindwa kura ya maoni kwa sababu ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo,” amesema.

Mkazi wa Mirongo wilayani Nyamagana, Juma Isihaka amesema ana imani na wote wawili kwa kuwa wamewahi kuongoza Nyamagana, akidai yeyote kati yao atayeteuliwa na chama chake kugombea kwenye jimbo hilo kwake ni sawa.