Wenje aeleza alivyokimbia Tanzania akiwa na kaptura

Muktasari:

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Ezekiel Wenje na mjumbe wa Kamati kuu ya Chadema amesema alitoroka nchini mwaka 2020 baada ya Uchaguzi Mkuu, akiwa amevaa kaptura na kwa mara ya kwanza alifikia hatua ya kuomba nguo za kuvaa.


Arusha. Aliyekuwa Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje na mjumbe wa Kamati kuu ya Chadema amesema alitoroka nchini mwaka 2020 baada ya Uchaguzi Mkuu, akiwa amevaa kaptura na kwa mara ya kwanza alifikia hatua ya kuomba nguo za kuvaa.

Wenje ametoka kauli hiyo Leo, Machi Mosi, 2023 wakati wa mkutano wa kumpokea aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema uliofanyika katika uwanja wa Relini jijini Arusha.

Wenje amesema alikuwa na Lema nchini Canada lakini yeye aliwahi kurudi nchini kusoma mazingira na kuangalia hali ya amani ilivyo.

"Mimi nilirudi mapema kidogo kusoma ramani lakini baada ya kuona hakuna tatizo ndio nikawashauri kina Lema nao warudi" amesema

Mwanasiasa huyo amesema kuondoka nchini na kurudi sio makosa kwani hata mwanamuzi Bob Marley aliwahi kuimba ni bora yule ambaye anapigana na akiona ameishiwa nguvuĀ  akaacha na siku nyingine akafanya hivyo akiwa na nguvu mpya.

Wenje alimshukuru aliyekuwa mgombea urais wa Kenya mwaka jana, Profesa George Wajackoyah wa chama cha Root kwa msaada mkubwa aliowapatia walipokuwa Kenya na baadaye Canada

Profesa Wajackoyah pia ni miongoni mwa wageni waalikwa ambaye pia amepata fursa ya kuhutubia katika mkutano huo.