Chadema yafungua milango watiania uchaguzi 2024, 2025

Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika akizungumza kwenye kongamano la Chama hicho lililofanyika jijini Mwanza leo. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Milango hiyo imefunguliwa leo na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kwenye kongamano la  chama hicho mkoani Mwanza huku akisema ametangaza hivyo ili kutoa fursa kwa chama hicho kuwapima wagombea wake kabla ya kuingia kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Mwanza. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimefungua rasmi milango kwa wanachama wake kuanza kutia nia ya kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho.

Milango hiyo imefunguliwa leo Alhamisi Desemba 29, 2022 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati wa kongamano la chama hicho mkoani Mwanza huku akisema ametangaza hivyo ili kutoa fursa kwa chama hicho kuwapima wagombea wake kabla ya kuingia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Amesema Chadema itapima utendaji kazi na utimamu wa wagombea hao kupitia ufanisi watakaoonyesha kwenye uhamasishaji wa wanachama wapya kujiunga na Chadema Digital, madai ya Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi aliyoitaja kuwa kiini cha kushinda katika uchaguzi huo.


"Kwa kuwa tunaingia kwenye mwaka wa uchaguzi wa ndani ya chama, vile vile kwa sababu mamlaka ya kufungua milango kwa watia nia amepewa katibu mkuu kutoa waraka, vile vile kwenye kanuni za chama bila hata kuandika waraka kauli ya katibu mkuu ni waraka ninatangaza kufungua milango kwa watia nia," amesema Mnyika


Pia, amewataka watia nia ngazi ya msingi, kijiji, kata, jimbo na hadi Taifa kufuata utaratibu wa kikatiba na kikanuni juu ya muongozo wa utiaji nia katika uchaguzi unaofanyika ndani ya chama hicho.


Mbunge huyo wa zamani wa majimbo ya Ubungo na Kibamba amesema, "tunataka wenye dhamira ya uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 tuwaone kwenye kazi ya Chadema Digital, Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi ili tuwapime uwezo na utayari wao kushiriki kwenye mapambano ya kisiasa ya ujenzi wa chama na madai ya Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi."


Amewataka wanachama wa Chadema kulishinikiza Bunge lipitishe muswada wa Katiba Mpya ili ujumuishwe katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/24 kwa ajili ya utekelezaji ikiwemo kutengewa fungu kwa ajili maandalizi ya kukamilisha mchakato huo.


"Maandalizi siyo ya kusubiria kwamba uchaguzi ufike ndiyo ujiandae kudai katiba mpya huo muda haupo, lazima tudai Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi wakati huo huo tunajiandaa na uchaguzi mkuu unaokuja ambao nao hatutafikia lengo iwapo hatuna Katiba Mpya," amesema


Awali, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche ameahidi kushiriki kujenga ngome imara ili kuyakomboa majimbo ya Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza huku akidokeza ili kufikia lengo la kukiondoa Chama Cha Mapinduzi madarakani wanachama wa Chadema takwa la Katiba Mpya haliepukiki.


"Wana Chadema nguvu tunazotunia kujadili Simba na Yanga tukiziweka kwenye maendeleo ya chama chetu, naamini CCM itaondoka madarakani mwaka 2025," amesema Heche


Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema, John Pambalu amesema amedokeza ongezeko la machinga ni ishara kuwa hakuna ajira kwa wananchi huku akishauri serikali kuja na sera ya vijana itakayoshinikiza kila Benki inayoanzishwa nchini kuwa dirisha la utoaji wa mkopo kwa vijana ili kuwawezesha kujiajiri.


"Tuwaone vijana kama rasilimali na siyo tatizo, ili utatue tatizo la ajira wape vijana mtaji na napendekeza katika kila Benki inayoanzishwa nchini kuwe na dirisha la kutoa mkopo kwa vijana," amesema Pambalu


Amesema sera hiyo inatakiwa iweke kipindi cha mpito kwa wajasiriamali na wafanyabiashara ili kutoa fursa kwao kujiimarisha kiuchumi kabla ya kuanza kulipishwa kodi jambo ambalo amesema sasahivi mtu anakadiriwa kodi ya biashara yake kabla ya kuanza kupata faida.


"Kuwe na kipindi cha mpito kwenye biashara, mfanyabiashara aende Halmashauri ajiandikishe wajue biashraa yake iko wapi, afanye kazi kwa miezi sita bila kulipishwa kodi, hapo hata aanguke asinguke watakuwa na haki ya kumlipisha kodi," amesema


Baada ya kumaliza kongamano hilo lenye lengo la kuhamasisha wanachama kujiunga na Chadema Digital, kudai Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi, Mnyika anaendelea na ziara yake katika Kanda ya Victoria ambapo kesho Ijumaa anatarajiwa kuwa Kahama mkoani Shinyana.