Saa 96 za Dk Chegeni kabla ya kutenguliwa

Dk Raphael Chegeni
Muktasari:
Ni saa 96 zimepita tangu Rais Samia Suluhu Hassan amteue mwanasiasa Dk Rapahel Chegeni kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na kisha kumtumbua bila kueleza sababu za kufanya hivyo.
Dar es Salaam. Ni saa 96 zimepita tangu Rais Samia Suluhu Hassan amteue mwanasiasa Dk Rapahel Chegeni kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na kisha kumtumbua bila kueleza sababu za kufanya hivyo.
Uamuzi wa kutengua uteuzi huo umezua maswali kadhaa kutoka kwa watu mbalimbali juu ya sababu za hatua hiyo zikiwa zimebaki saa chache kabla ya wateule hao kuapishwa leo.
Chegeni aliteuliwa kushika wadhifa huo uliokuwa ukishikiliwa na Ally Hapi ambaye sasa amewekwa kando.
Chegeni alipata kuwa mbunge wa Busega hadi mwaka 2020 ambako jina lake halikuteuliwa licha ya kuongoza katika kura za maoni ambapo alipata kura 209 kati ya 673 za wana CCM.
Katika kinyang’anyiro hicho Chegeni alimuacha mbali mpinzani wake, Dk Titus Kamani aliyepata kura 84, akifuatiwa na Simon Songe aliyepata kura 49 ambaye ndiye aliteuliwa na baadaye kushinda.
Taarifa iliyotolewa jana jioni na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zuhura ilieleza Rais Samia amemteua Meja Jenerali, Suleiman Mzee kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na kutengua uteuzi wa Chegeni.
Kabla ya uteuzi huo, Meja Jenerali Suleiman Mzee alikuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza na leo anatarajia kuapishwa katika hafla itakayofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kutengua uteuzi muda mfupi baada ya kuteua, kwani Aprili 5, 2022 alitengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Thobias Richard ikiwa ni chini ya saa 12 tangu amteue kushika wadhifa huo.Ingawa haikuwekwa wazi sababu za kufanya hivyo, ilidaiwa Thobias hakuwa na uzoefu mkubwa kulinganisha na Dk James Mataragio ambaye alirejeshwa kuendelea na wadhifa huo aliondolewa kwa takriban saa 12.
Uteuzi wa Mzee
Mzee aliteuliwa kushika wadhifa huo Juni 2020 na Rais John Magufuli, unatoa taswira kuwa Rais Samia anaendelea kufanya mabadiliko katika vyombo vya ulinzi na usalama ambapo siku chache zilizopita alimteua Camillius Wambura kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi akimuondoa Simon Sirro aliyemteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Rais Samia alisema amedhamiria kufanya maboresho katika vyombo vinavyotoa haki jinai na ameshaunda kamati ya watu 12 itakayoongozwa Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Othman Chande na sektarieti ya watu watano itakayokuwa chini ya Balozi Ombeni Sefue ambayo itakuwa na jukumu la kutathimini mwenendo wa vyombo hivyo na kumshauri namna bora ya kuboresha utendaji wake.