Saba wajeruhiwa basi la New Force likiligonga lori

Songwe. Abiria saba waliokuwa wanasafiri katika basi la Kampuni ya New Force (Golden Deer) lililokuwa likitoka Tunduma kwenda Dar es Salaam wamejeruhiwa baada ya basi hilo kuligonga lori lililokuwa limeegeshwa katika eneo la Ruanda wilayani Mbozi mkoani Songwe.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, ACP Theopista Mallya amesema ajali hiyo imetokea leo Juni 6, 2023 alfajiri ambapo basi hilo la Kampuni ya Golden Deer imeligonga lori kwa nyuma aina ya Scania.
"Bus hilo limetonga lori alfajiri ya leo maeneo ya Ruanda Mbozi dereva na konda wameumia na ni miongoni mwa majeruhi saba wa ajali hiyo ambao wote wamepelekwa katika Hospitali ya Wilaya Mbozi na abiria wengine wameendelea na safari," amesema Kamanda Mallya.
Amewataja majeruhi waliofikishwa hospitalini kuwa ni Sakina Ramadan (45) Raia wa Congo DR, Lemmy Mkonde (48) Raia wa Zambia, Solomon Michael (36) mkazi wa Tunduma, John Felix (24) mkazi wa Dar es alaam, Geoffrey Swai ambaye Mkazi wa Tunduma, Mpuyi Tita (34) mkazi wa Kasumbalesa Congo na Frank Chilobi (37) mkazi wa Dar es Salaam.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Jailo Shitindi amesema ajali hiyo imetokea wakati basi hilo likijaribu kulipita lori lililokuwa limesimama ndipo dereva wa basi hilo aliliona lori lingine likija mbele yake ndipo alilazimika kurudi upande wake na wakati huo akawa amelifikia lori lililosomama.