Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu meli ya New Mv Victoria kusitisha safari yatajwa

Muonekano wa meli ya New Mv Victoria 'Hapa Kazi Tu'.

Muktasari:

  • Meli hiyo iliyosimama kufanya safari kati ya Mwanza na Bukoba kupitia bandari ya Kemondo mkoani Kagera tangu Machi 11, 2025, inatarajiwa kuanza tena safari Mei 22.

Mwanza. Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico) imetangaza kuwa kusimamishwa kwa safari za meli ya New MV Victoria ‘Hapa Kazi Tu’ kwa kipindi cha miezi miwili kulitokana na matengenezo makubwa yaliyolazimika kufanyika kwa mujibu wa sheria za kimataifa za usalama wa meli.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa matengenezo hayo ni sehemu ya matakwa ya kimataifa ya kuhakikisha usalama wa meli, abiria na mizigo, sambamba na kuhakikisha ufanisi wa meli hiyo katika utoaji wa huduma za usafirishaji katika Ziwa Victoria.

Kauli hiyo imetolewa baada ya malalamiko ya wakazi wa Kanda ya Ziwa wanaoitumia meli hiyo inayofanya safari kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Kemondo mkoani Kagera ambayo ilisimama kufanya safari hizo  kuanza Machi 11, 2025.

Akizungumza baada ya kukagua meli hiyo leo Jumanne Mei 20, 2025 Mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza, Michael Lushinge 'smart' amesema kusimama kwa meli hiyo imekuwa kero kwa wananchi na amekuwa akipokea malalamiko mengi.

Mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza, Michael Lushinge 'smart' akizungumza na waandishi wa habari kuhusu meli ya New Mv Victoria 'Hapa Kazi Tu'.

"Sisi viongozi wa chama tumepata malalamiko mengi...ilikuwa ni kero hii meli kusimama kufanya safari ilileta  usumbufu mkubwa.

"Dhamira ya CCM ni kuhudumia wananchi na kutatua kero zao,  Rais Samia Suluhu Hassan ndiyo kazi kubwa anayoipigania kuhakikisha changamoto zote za wananchi zinatatuliwa," amesema mwenyekiti huyo.

Amesema baada ya kuikagua amehakikishiwa itaanza safari zake Mei 22, 2025 baada ya kumalizika matengenezo makubwa iliyokuwa ikifanyiwa.


 Sababu za kusimama kutoa huduma

Nahodha Mkuu wa meli hiyo, Adam Mwisungu amesema ilisimama kutoa huduma ili kupisha matengenezo makubwa ya sheria za kimataifa yanayoelekeza meli zinazobeba abiria kufanyiwa uchunguzi.

 "Zinatuelekeza sisi kusimamisha meli kwa ajili ya uchunguzi hususan hizi zinazobeba abiria na mizigo. Kwa hiyo ilisimama kutekeleza matakwa ya sheria,"amesema.

Ameongeza kuwa pia meli ilikuwa inahitaji marekebisho katika upande wa majembe ya kukatia maji (propera) ..propera ilikuwa ina hitilafu kidogo tukaona ni vema tukaisimamisha tukafanya matengenezo makubwa kuanzia mwanzo mpaka mwisho ili meli irudi kama mpya," amesema.

Ametaja baadhi ya marekebisho yaliyofanyika ni matengenezo makubwa ya injini ambayo yatafanya spidi ya meli kuongezeka kutoka knot 12.5 hadi kufikia knot 14.8, hivyo itatembea saa saba badala ya saa tisa za awali.

"Awali tulikuwa tukitumia saa nane kutoka Mwanza mpaka Kemondo na kutoka Kemondo hadi Bukoba tulikuwa tunatumia saa moja, kwa hivyo jumla ya saa tisa. Kwa sasa hivi kwa hii spidi tunaweza tukatumia saa saba au sita na nusu lakini tutaenda na spidi ya kawaida ambayo ni salama," amesema.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma Tashico, Anselm Namala amesema; "Itarejea Mei 22, 2025 iking'oa nanga bandari ya Mwanza kuelekea Bukoba ikipitia Kemondo baada ya matengenezo ya miezi miwili.

"Inarejea ikiwa imenakshiwa, viti vimerekebishwa, upande wa burudani pia pamerekebishwa.”