Sababu mkutano wa rasilimali watu kufanyika Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax.
Muktasari:
- Tanzania inakuwa nchi ya kwanza katika Bara la Afrika kuwa wenyeji wa mkutano wa rasilimali watu.
Dar es Salaam. Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa Wakuu wa nchi wa Afrika utakaojadili kuhusu uwekezaji katika rasilimaliwatu.
Mkutano huo utakaofanyika Julai 25 na 26 mwaka huu, utahusisha Wakuu wa nchi mbalimbali za Afrika na Mawaziri wa sekta za rasilimali watu.
Hii ni mara ya kwanza mkutano huo kufanyika nchini na katika bara la Afrika kwa ujumla.
Taarifa kuhusu mkutano huo, imetolewa leo Julai 17 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax.
Kuimarika kwa amani, amesema ni miongoni mwa sababu za Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Sababu nyingine za Tanzania kuchaguliwa ni hatua ilizochukua katika kuwaendeleza vijana ikiwemo kuimarisha sekta za elimu na afya.
"Tanzania iliombwa kuwa mwenyeji wa mkutano na vigezo ni kwamba Tanzania ni moja ya nchi za Afrika ambazo idadi ya watu inakuwa kwa kasi na ina hazina kubwa ya vijana," amesema.
Kamishna wa Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha, Richard Bade amesema hatua ya Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo, ilitokana na kuombwa na Benki ya Dunia.
Amezitaja sababu nyingine za Tanzania kuombwa ni ongezeko la idadi ya watu hasa vijana na uwezo wake wa kutumia mtaji wa vijana katika maendeleo.
Katika hatua nyingine, Dk Tax ametangaza ziara ya Rais wa Hungary nchini Tanzania, Katalin Novák anayetarajia kuwasili leo usiku.
Amesema Rais huyo ambaye ni wa kwanza mwanamke nchini humo, baada ya kuwasili nchini kesho yake atakutana na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
"Baada ya kukutana watafanya mazungumzo ya siri baadaye watafanya mazungumzo ya kiserikali na kisha watazungumza na waandishi wa habari," amesema.
Baada ya mkutano na waandishi wa habari, amesema Rais Katalin atakwenda mkoani Arusha na kutembelea vivutio mbalimbali na atasafiri kurudi kwao kupitia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro.